Waziri,Ofisi ya Rais Menejimenti na Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama akizindua Mfumo wa kielektroniki wa tathimini ya Hali ya Rasilimali watu katika Utumishi wa Umma.
Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti na Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama akizungumza na waandishi wa habari .
Na Asha Mwakyonde, Dodoma
WAAJIRI wote wametakiwa kusimamia Wakurungenzi,Wakuu wa Idara na sehemu zote zinazosimamia rasilimali watu na taasisi zao ili wakamilishe zoezi la mfumo wa Kielektroniki wa Tathimini ya Hali ya Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma.
Agizo hilo limetolewa leo Machi 24 2022,na Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama wakati akizindua Mfumo huo amesema unawarahisishia kufanya kazi.
Amesema mfumo huo umesanifiwa na kujengwa na wataalamu wa ndani ya ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa umma na utawala Bora.
Waziri huyo ameeleza kuwa jambo hilo sio dogo kwa serikali kwani wasingekuwepo wataalamu hao ambao wamejenga mfumo huo wa kielektroniki ingewapasa kutafuta wataalamu elekezi na wajengaji wa mfumo huo kutoka nje ya nchi na wangeweza kutumia gharama kubwa.
" Timu hii imeweza kufanya kazi mchana na usiku kufanikisha mfumo huu, nawapongeza na kuwashukuru Sana," amesema Waziri Mhangama.
Amesema watahakikisha wanautunza mfumo huo ili ufanye kazi kwa muda mrefu na kwamba ofisi ya Rais Menejimenti na utumishi wa umma na utawala Bora uliichukua mfumo wa Kielektroniki na kupeleka katika Taasisi za Umma.
Waziri huyo amesema kuwa bado kuna taasisi za Umma chache zilizopo nje katika Mfumo wa kiutumishi lakini pia zilipelekewa nyenzo maalumu ya kidigitali ya kukusanya taarifa ambazo zitachakatwa kwa mfumo wa Kielektroniki na kuingizwa kwenye mfumo huo ulizinduliwa.
Amesema mfumo umebaini taasisi 94 ambazo hazijafanya vizuri katika kuingiza taarifa kwenye mfumo huo kwa kuwa zipo chini ya wastani wa asilimia 50 katika kutekeleza matakwa ya zoezi hilo.
Waziri huyo amesema lengo la uzinduzi wa mfumo huo ni kwa kuwa unakazi kubwa ya kusanifu na kuujenga mfumo, kulisaidia taifa, serikali kupata fursa ya kufanya tathimini ya kutosha yakina yenye kisayansi, yenye ubobezi ya hali ya watumishi wa Umma kwa idadi iliyopo na majukumu ambayo wanayo katika vituo ambavyo wanafanyia kazi.
Amebainisha kuwa mfumo huo utafanya kazi ya kimsingi ya kufanya thathimi ya hali ya watumishi katika taasisi za utumishi wa Umma.
"Ofisi ya Rais, Menejimenti na utumishi wa Umma na utawala Bora ina majukumu kadha wa kadha ikiwa ni pamoja na majukumu ya kisera na kiutendaji yanayotekelezwa na yanapo tekelezwa yanatazingatia kanuni, taratibu na miongozo lakini yote haya ni katika kulenga usimamizi wa rasilimali watu tangu mtumishi anapoajiriwa hadi pale anapostaafu kwenye utumishi wa umma," amesema.
Amesema kuwa wanawajibu mkubwa wa kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan katika kutimiza majumu yake na kuhakikisha anafanikisha juzudi zake.
Ameongeza kuwa kazi yao ni kuhakikisha usimamizi wa rasilimali watu na kwamba bila kuwa na rasilimali watu wenye viwango juhudi za Rais Samia hazitaweza kufanya kazi vizuri hivyo wanawajibu hasa kwa wao wanaosimamia rasilimali watu nchini.
Waziri Mhagama amesema katika kutekeleza majukumu aliyopangiwa watahakikisha wanatembea katika dira ya Maendeleo ya Taifa na Ilani ya uchaguzi ya chama Cha Mapindizi (CCM), kwa kipindi hiki husika na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano.
"Wote mnajua kuwa hizi ndo nyenzo kuu katika kujipanga lakini sisi ofisi ya Rais Menejimenti na utawala Bora tutakwenda kutembea katika maono ya Rais Samia ambaye tangu awali alitambua maono yake katika sekta ya Umma," ameeleza.
Waziri Mhagama amefafanua kuwa Rais Samia anatamani uendeshaji wa watumishi wa Umma nchini uwe wa kidigitali wahame huko na kuendesha utumishi huo kwa mifumo ambayo watakuwa wameijenga itakayowezesha kutimiza wajibu wake sawa sawa.
Amesema pia mfumo huo Rais Samia anatamani ufanye kazi katika kutenda haki kwa pande zote mbili mwajiri na mwajiriwa na unaozingatia uzalendo.
0 Comments