SERIKALI YATANGAZA AJIRA MPYA PAMOJA NA KUPANDISHA VYEO WATUMISHI 92,619


 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani), wakati akitangaza nafasi mpya za ajira.

Baadhi ya waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama (hayupo pichani), wakati akitangaza nafasi mpya za ajira.

Na Asha Mwakyonde, Dodoma

 

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama leo ametangaza   ajira mpya 44,096,itayoigharimu serikali shilingi bilioni26.297 kwa mwezi sawa na Shilingi bilioni 315.570 kwa mwaka katika utekelezaji wake.

Pia Waziri Mhagama amesema kuwa serikali imewapandisha vyeo watumishi  92,619 pamoja na kubadilisha kada watumishi 6,026  kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

 

Waziri Mhagama ameyasema hayo leo April 12, 2022 jijini hapa  wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuhusu utekelezaji wa ahadi ya Serikali  ya kuajiri watumishi wapya, amesema sekta zilizopewa kupaumbele ni Elimu na Afya .

Waziri huyo amefafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2021/22 Serikali iliidhinishiwa nafasi 44,096  za ajira mpya, nafasi  92,619 za kupandisha vyeo watumishi  pamoja na kuwabadilishia kada/vyeo (Re-categorization)  watumishi 6,026  kwa kada mbalimbali.

 

‘Kati ya nafasi 44,096  za Ajira mpya, Serikali kupitia Taasisi zinazotumia Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara imeshaajiri watumishi 12,336  wakiwemo watumishi 11,492wa ajira mpya na watumishi 844 wa ajira mbadala  hadi sasa na watumishi hawa wanaendelea kutekeleza majukumu yao katika taasisi mbalimbali za umma.’ Amesema.

Mhagama ameeleza kuwa taarifa hiyo ni hatua ya kwanza ya mchakato wa kuhakikisha utekelezaji wa ajira hizo unakamilika kabla ya mwaka wa fedha 2021/22 haujaisha.

‘Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan,katika kuhakikisha Taifa linapata maendeleo ya haraka ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya ujenzi wa uchumi na inayotoa huduma iliyoasisiwa na Serikali zilizopita na ile iliyoanzishwa na inayoendelea kutekelezwa ikiwemo Miradi ya UVIKO 19, ambapo Serikali imetoa kipaumbele katika Sekta za Elimu, Afya.

Ameongeza kuwa mbali na sekta hizo Serikali imezingatia mgawanyo wa ajira katika Sekta nyingine zikiwemo Kilimo, Maji, Mifugo, Uvuvi pamoja na maeneo mengine yenye uhitaji     wa watumishi.

Mhagama amesema kuwa kwa upande wa watumishi wanaopandishwa vyeo,Serikali itawapandisha vyeo au madaraja watumishi 92,619  ambapo itatumia jumla ya Shilingi bilioni23.078 kwa mwezi sawa na Shilingi bilioni 276.938 kwa mwaka na kuwabadilisha vyeo/kada (Recategorization) watumishi 6,026waliotengewa Ikama na Bajeti ya Mishahara kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 kuanzia Mei Mosi mwaka huu  kwa gharama ya Shilingi milioni824. 441 kwa mwezi sawa na Shilingi bilioni 9.893 kwa mwaka. 

‘‘Kwa kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan  jumla ya watumishi wa umma 282,400watakuwa wamepandishwa vyeo katika kipindi hiki kifupi…., Aidha, jumla ya watumishi 25,412 watakuwa wamebadilishiwa kada katika kipindi tajwa.’’

Ameziagiza Mamlaka za Ajira, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Wizara ya Afya pamoja na Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma kuhakikisha wanaendesha michakato ya ajira hizo kwa uwazi, weledi, uadilifu pamoja na kutoa fursa sawa kwa waombaji wote kuweza kushiriki katika mchakato huo na hatimaye Serikali iweze kupata watumishi mahiri na wenye sifa stahiki.

Aidha amewataka waajiri kutotumia fursa hiyo kuajiri watumishi wazembe au wasiotekeleza majukumu yao kikamilifu kwa lengo la kujaza nafasi kwani jambo hili halikubaliki na halitavumiliwa kwa namna yeyote.

Alisema, Ofisi yake itafuatilia mchakato mzima wa ajira hizo hatua kwa hatua ili kuhakikisha Serikali inapata watumishji wenye sifa na ubora ambao wapo tayari kulitumika Taifa.



Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU