Na Asha Mwakyonde, Dar es Salaam
SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),yang'ara na kupata tuzo ya ushindi baada ya kuibuka mshindi katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, maarufu kama Sabasaba, kwa kulinda mazingira kupitia matumizi ya nishati safi.
Akizungumza kwa furaha leo Julai 7, 2025 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka TPDC, Maria Mselemu, ameeleza kuwa hiyo ni tuzo ya tano katika maonesho hayo.
Ameongeza kuwa Shirika hilo limekuwa ni kawaida kupata tuzo kutokana na ubora wa huduma na miradi yao na kwamba kupitia matumizi ya nishati safi wameweza kuondoa zaidi ya tani 100,000 za hewa ukaa.
Mkuu huyo wa kitengo ameeleza kuwa hiyo ni hatua kubwa katika kulinda mazingira na kwamba wanajivunia kuwa sehemu ya suluhisho la mabadiliko ya tabianchi.
Amesema TPDC imefanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa utoaji wa hewa ukaa kwa kutumia nishati safi ya kupikia na ile inayotumika katika magari, hatua ambayo imechochea mafanikio yao katika nyanja za mazingira.
0 Comments