Na Asha Mwakyonde
DAKTARI, Bingwa wa Uzazi na Magonjwa ya Wanawake kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili ( MNH), Dk.Nathanael Mtinangi amesema tatizo linalojulikana na linaloambatana na Fistula ambalo kitaalamu huitwa Foot drop husababishwa na mguu mmoja au yote kupata udhaifu baada ya kukandamiza kwa muda mrefu mishipa ya fahamu (Perineal nerve), wakati wa kujifungua.
Daktari huyo ameyasema hayo wakati wa mahojiano na chombo hiki jana lengo likiwa ni kutaka kufahamu namna ya kupata tiba baada ya tatizo la Foot drop, Dk.Mtinangi amesema ni kufanya mazoezi (Physiotherapy), na kwamba inategemea ni kwa muda gani kutokana na mshipa ulivyoharibika.
Dk.Mtinangi ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Uzazi na Magonjwa ya Wanawake kutoka hospitali ya Muhimbili amesema kuwa tatizo hilo haliendani na umri bali linawapata akina mama wote ambao wanajifungua.
"Pamoja na tatizo hili kutokea kwa akina mama hakuna utafiti uliofanyika kuonyesha kuwa wanawake wanapojifungua hupooza, amesema daktari huyo.
Pia ameongeza kwamba ni vema akina mama kuanza kliniki mapema ili Wataalamu wa vituo vya Mama wajawazito wabaini viashiria hatarishi kwa lengo la kuweza kufanyiwa upasuaji endapo amepata uzazi pingamizi ambao unasababisha mishipa ya fahamu kuumia.
0 Comments