Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dk.Geofrey Mkamilo akisaini kitabu cha wageni baada ya kutembelea banda la taasisi hiyo.
Na Asha Mwakyonde
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania(TARI),Dk.Geofrey Mkamilo,amesema kuwa taasisi hiyo ina mkakati mkubwa wa kuhakikisha Teknolojia zote zinamwendea mkulima.
Dk. Mkamilo ameyasema hayo Julai 9,2022 katika Maonyesho ya 46 ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu Saba Saba yanayaofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere wakati alipotembelea banda la TARI, amesema wapo kwenye maonyesho hayo kutoa elimu kuhakikisha wakulima wanapata teknolojia pamoja na wanafahamu fursa zilipo hapa nchini kupitia kilimo.
Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa lengo ni kuhakikisha wakulima hao wanazitumia fursa hizo ili nchi isiwe tegemezi bali iwe na chakula cha kujitosheleza.
Amesema kwa Agenda 10/30 ifikapo mwaka 2030 mchango wa Kilimo utakuwa umefikiwa kwa asilimia 10 ikilinganishwa na sasa na kwamba chochote kitafanyika pale watakapokuwa na teknolojia sahihi ambazo zimegunduliwa na Wizara ya Kilimo kupitia taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania.
"Tuna vituo mahiri 17 nchi nzima na hivi ni vituo mahiri kwa kusimamia mazao mahiri ya kimkakati kwa lengo la kuhakikisha kuna kuwa na chakula cha kujitosheleza lakini pia kiweze kuchangia uchumi wa nchi katika Taifa letu," ameeleza Dk. Mkamilo.
Kwa upande wake mkazi wa Mbezi Luis Juma Ndaki aliyetembelea banda la TARI amesema kuwa amepata elimu kuhusu kilimo chenye tija.
" Nimekuja hapa kuangalia aina mbalimbali za mazao. Nataka kufanya kilimo cha kitaalamu zaidi kwa kuwa kuna wataalamu hapo ni fursa ya kipekee, wamenipa ushauri wa Kilimo nimepata huduma nzuri hasa kujua aina ya udongo unaofaa kwa zao lipi" amesema Ndaki.
Ameongeza kuwa anaamini baada ya kuapata elimu hiyo ataenda kuanza uwekezaji wa kilimo huku akisema mara nyingi watu wamekuwa wakilima bila mafanikio kwa kukosa elimu.
0 Comments