Na Asha Mwakyonde, Dar es Salaam
MKUU wa Maabara Kuu ya Udongo Tanzania, Mkoa wa Tanga kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Mlingano Dk.Kobusinge Aloys amesema kuwa uchukuaji wa sampuli za udongo unahitaji mtu sahihi anayeweza kuchukua sampuli hiyo ambayo ni wakilishi kwa shamba zima.
Akizungimza hivi karibuni katika Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu Saba Saba yaliyofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini hapa, Mkuu huyo wa Maabara amesema wanashauri sampuli ya udongo ili iweze kuchukuliwa vema ni vizuri kupata watu sahihi wa kuchukua udongo huo kwa lengo la kuepuka kuathiri majibu ya mwisho yanayopatikana katika uhakiki wa vipimo.
Dk. Kobusinge ameeleza kwamba kabla ya kuanza uwekezaji wa kilimo mwekezaji, mkulima anatakiwa kupeleka sampuli ya udongo katika maabara hiyo ili kuangalia Afya ya udongo kwenye shamba lake.
Ameongeza kuwa vitu vingine wanavyoangalia katika afya ya udongo ni pamoja na chimvi na tindikali.
"Shamba linaweza kuwa kubwa au dogo lakini ndani ya shamba kuna aina tofauti ya udongo linaweza kuwa na udongo wa kichanga au mfinyanzi ndio maana tunashauri sampuli ichukuliwe na mtu sahihi anayefahamu vizuri masuala ya udongo," amesema.
Dk. Kobusinge amefafanua kuwa wanaangalia hali ya udongo je virutubisho vipo chini, juu au vipo sahihi kulingana na zao husika linalotakiwa kulimwa katika shamba hilo.
" Kwa kuwa hii ni kazi ya serikali mwekezaji, mkulima atapatiwa namba ya kulipia baada ya kulipia sampuli ya udongo wake itafanyiwa uhakiki na kupatiwa majibu pamoja na ushauri ni nini afanye ndani ya shamba lake kulingana na mahojiano ambayo tumefanya na mwekezaji na kugundua anahitaji kufanya kilimo cha aina gani," ameeleza.
0 Comments