RAIS SAMIA KUZINDUA MUONGOZO WA MATUMIZI YA MATOKEO YA SENSA


 NA ASHA MWAKYONDE, DODOOMA


RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua Muongozo wa matumizi wa matokeo ya sensa ya watu na makazi mara baada ya kutangaza matokeo ya Sensa ambayo imefanyika Agosti 23 mwaka huu.

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera,Bunge na Uratibu George Simbachawene amesema muongozo huo ni muhimu kwani matokeo hayo yakipatikana kinachofuata ni matumizi.

 

Amesema kuwa takwimu zitakazopatikana zitasaidia katika shughuli mbalimbali za kupanga mipango zikiwamo taasisi za Umma, binafisi hata wafanyabiashara huku akisema kwa upande wa serikali bila takwimu hizo haitapanga Mipango yake.

 

Waziri Simbachawene ameongeza kuwa wanahitaji takwimu ili waweze kupanga mipango ya serikali zikiwamo huduma za kijamii kama maji, umeme, hospitali, masuala ya kilimo na nyinginezo.

 

"Kama ambavyo tumewatangazia hivi karibuni, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imo katika maandalizi ya Uzinduzi wa Matokeo ya Mwanzo ya Sensa ya Watu na Makazi, Sensa ya Majengo na Sensa ya Anwani za Makazi ya Mwaka 2022 utakaofanyika katika uwanja wa Michezo wa Jamhuri hapa jijini Dodoma"

 

Katika uzinduzi huo kama mlivyoelezwa katika taarifa zetu mbalimbali, Mgeni Rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

 

Simbachawene amesema, Sensa ya Watu na Makazi hufanyika mara moja kila baada ya miaka kumi na matokeo yake ndio yanayotumika katika kufanya maamuzi yote muhimu yanayohusu maendeleo ya nchi kwa kipindi cha miaka kumi hadi Sensa nyingine.

 

 "Hivyo, uzinduzi huu ni tukio moja muhimu katika historia ya maendeleo ya nchi hivyo ndio maana Serikali imeamua kuhakikisha kunakuwa na uwakilishi wa wananchi wa makundi yote ili waweze kushiriki katika tukio hili la kihistoria,

 

"Matokeo haya ni muhimu sana kwa makundi yote katika jamii, wafanyabiashara, wakulima, wafugaji na hasa kwa Serikali yetu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwani Serikali itaweza kupanga mipango yake kwa ajili ya maendeleo ya wananchi kulingana na idadi, mahitaji na mazingira wanamoishi" Amesema Simbachawene 

 

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Zanzibar anaeshughulikia Sera Bunge,Uratibu, na Baraza la wawakilishi Hamza Hassan Juma amesema zoezi hilo lilienda vizuri kwa upande wa Zanzibar na taarifa zilizopatikana zitasaidia kujua idadi ya watu kujua kasi ya ukuaji kwa baadhi ya Mikoa .

 

" Takwimu hizi zitatusaidia sana na hasa Katika masuala ya utafiti wenzetu wanaofanya tafiti zitasaidia kujua wanatafiti kwa watu wangapi" amesema Hamza.

 

Tarehe 31 mwezi October Rais Samia Suluhu Hassan atatangaza matokeo ya mwanzo ya sensa ya watu na makazi hapa jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na Marais wastafu wa jamhuri ya Muunganio wa Tanzania huku hafla hiyo ikiambatana na burudani mbalimbali.

 

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU