SERIKALI YAOKOA ZAIDI BILIONI 2.3 HUDUMA ZA UPANDIKIZAJI FIGO NCHINI


 NA ASHA MWAKYONDE,DODOOMA

HOSPITALI ya Benjamin Mkapa ( BMH),
imeanza kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto waliobainika kuwa na matatizo ya kuzaliwa ya moyo, tayari watoto kumi wameshahudumiwa.

Pia Serikali imeokoa zaidi ya Shilingi bilioni 2.3 kutokana na  huduma za upandikizaji wa figo  kwa wagonjwa 31 ambao wametibiwa kwa gharama ya Shilingi milioni 25 ambapo wangeenda kutibiwa nje ya nchi ingegharimu milioni 100 kwa mtu mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Oktoba 26, 2022, Dk. Alphonce Chandika wakati akitoa taarifa ya utekelezaji na vipaumbele vya hospitali hiyo kwa mwaka 2022/ 2023 amesema wamefanikiwa kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa kuwa kuna  maabara maalum inayotumika katika kutoa matibabu ya moyo pasipo kufungua kifua. 

Dk. Chandika ameeleza kuwa kuna wagonjwa nane ambao mapigo yao ya moyo yanashuka sana, walihudumiwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kupandikizwa betri kwenye moyo na kupitia maabara hiyo tumeweza kuhudumia watoto 14 waliozaliwa na matatizo ya moyo.

Amesema wagonjwa 39 waliobainika kuwa na matatizo makubwa ya moyo wamehudumiwa kwa kuwekewa vipandikizi na kati ya 39, wagonjwa wawili kati yao walihudumiwa kwa dharura ambapo kama ingekuwa ni kusafirishwa kwenda kupatiwa matibabu Dar es Salaam wangepoteza maisha. 

"Hospitali hii imejikita katika kuanzisha na kuboresha huduma za ubingwa bobezi ambapo imefanikiwa kuanzisha huduma za upandikizaji wa figo," amesema.

Ameongeza kuwa hospitali BMH ni ya pili hapa nchini kutoa huduma hiyo na kwamba tangu  mwaka 2019,  na kwamba jumla ya wananchi 715 wamehudumiwa kwa kuchunguzwa.

Daktari huyo amebainisha kuwa tangu mwaka 2020, Hospitali ilifanikiwa kuanzisha upasuaji wa nyonga na magoti kwa kuweka vipandikizi na tayari wagonjwa 56 wamewekewa vipandikizi hivyo kwa wastani wa gharama ya shilingi milioni 12 ambapo  gharama za huduma hizo nchi za nje ni takriban milioni 35.

"Wagonjwa hawa 56 tuliowahudumia,  Serikali imeokoa kiasi cha Shilingi bilioni 1.28, hospitali hii ndio pekee nchini imefanikiwa kuanzisha huduma ya uvunjaji wa mawe kwenye figo kwa kutumia mawimbi na miale pasipo kumfanyia  mgonjwa upasuaji," amesema.

Aidha ameongeza kuwa  huduma hiyo imeshatolewa kwa wagonjwa 148 kwa gharama ya Shilingi milioni 1.2 kwa mgonjwa mmoja, kwa nje ya nchi gharama ni zaidi ya milioni 7 huku akieleza kwamba wagonjwa hao 148,  Serikali imeokoa zaidi ya Shilingi milioni 850.

Ikumbukwe kuwa jitihada za Serikali kuhakikisha inawaletea wananchi huduma za afya zilizo bora, ilidhamiria kuiwezesha Hospitali ya Benjamini Mkapa kuwa na  vifaa tiba vya kisasa na vinavyotumia teknolojia ya kisasa ili iweze kukidhi adhma yake ya kuwahudumia wananchi hao kwa kuwapatia matibabu ya kiwango cha juu.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI