DK.GWAJIMA: IKIUNDWA SHERIA YA USTAWI WA JAMII ITARAHISISHA UTETEZI WA HAKI ZA MAKUNDI MAALUMU


 Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na Maafisa Ustawi wa Jamii wakati akifungua Mkutano wa Mwaka Chama cha wa Maafisa Ustawi wa Jamii (TASWO), jijini Dodoma Oktoba 26, 2022.

Baadhi ya Maafisa Ustawi wa Jamii kutoka mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa wakifuatilia ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa Chama cha Maafisa Ustawi wa Jamii jijini Dodoma Oktoba 26, 2022. 

NA ASHA MWAKYONDE, DODOMA

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk. Dorothy Gwajima amesema  uwepo wa watoto wanaoomba mitaani unawanufaisha watu wachache wanaowatumia watoto hao na kuzinufaisha familia zao.

Pia  amewataka maofisa Ustawi wa Jamii kufanya utambuzi wa watoto katika maeneo yao ili kuzuia watu wanaowatumia  watoto hao kwa shughuli zisizofaa.

Akizungumza katika mkutano wa wanataaluma, wataalam na wadau wa Ustawi wa Jamii Dk. Gwajima amesema
 watoto hao  wakiomba kwa siku wanapata Shilingi 10,000 au 15,000  hivyo miaka mitatu  wanakusanya fedha nyingi.

"Unaweza kujiuliza kwa muda wa miaka mitatu wanapata kiasi gani cha fedha?. Na wanaweka kwenye benki gani kama siyo kutumika kama miradi ya watu, amehoji " Dk. Gwajima.

 Aidha Dk. Gwajima amewaagiza Maofisa hao kuwa na daftari maalum la watoto ambalo litaainisha changamoto za kila mmoja na wale wenye mahitaji maalum na wasiokuwa wasiokuwa na makazi wapelekwe kwenye makazi maalum.

"Kila mmoja  akitimiza wajibu wake kusimamia  pale alipo hakutakuwapo na suala la watoto waliopo katika mazingira yasiyokuwa rasmi na  kujiingiza katika suala la kuomba mitaani," ameeleza Dk. Gwajima.

Dk. Gwajima amesema Sheria ya Ustawi wa Jamii ikiundwa itarahisisha Uratibu wa utetezi wa haki za Makundi maalum.

Amesema Maafisa Ustawi wa Jamii hawajapata Sheria ya kitaaluma inayowezesha kufanya kazi kama madaktari wa Jamii hivyo kutokuwa na Baraza la Ithibati kwa watoa Huduma za Ustawi wa Jamii.

Waziri Gwajima amesema Serikali inaendelea kutafuta fedha zaidi ili kujenga vituo zaidi huku akisema
vipo vituo 30 vya malezi vilivyojengwa na wadau ambavyo vimekuwa msaada mkubwa kwa jamii.

Aidha Waziri Gwajima amesema maofisa Ustawi wa Jamii ni madaktari wa Jamii na wanahitajika katika kila eneo lenye ikiwemo kwenye nyumba za Ibada.

Amesema hata katika masuala ya afya ya akili ambayo yametajwa kuongezeka katika siku za karibuni maofisa Ustawi pia wanahusika katika kutoa unasihi na kupunguza changamoto hiyo ambayo amewataka kutafuta chanzo cha ongezeko lake.

Waziri Gwajima amesema kutokana na kuwepo kwa uhusiano baina ya afya ya akili na matumizi ya Dawa za kulevya maofisa hao wanapaswa pia kushiriki katika vita ya dawa za kulevya.

Amebainisha kuwa amesema wakati wa kutokomeza vitendo hivyo umefika kwa kutoa elimu na kufanya kazi karibu na jamii ili wanajamii wafunguke wanapokutana na changamoto ili kukomesha vitendo vya ukatili.

Waziri huyo amesema sheria ya Ustawi  ni ya muhimu maana itafanya utambuzi wa wana taaluma ya Ustawi na kutoa Ithibati na leseni kwa wanataaluma hao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Ustawi wa Jamii nchini (TASWO),Dk.Mariana Makuu ameeleza kuwa wamekuwa wakiona jitihada za makusudi zinazofanywa na Serikali na  wadau katika kutatua changamoto mbalimbali zinaoikabaili jamii ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa mazingira bora na wataalamu kuendelea kufanya kazi ya kuimarisha Ustawi wa Jamii.

Aidha Mwenyekiti huyo ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Ofisi ya Rais TAMISEMI  kwa kushirikiana na TASWO katika kuboresha mazingira ya utoaji wa Huduma mbalimbali.


Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI