Na Asha Mwakyonde, DODOMA
TANZANIA Agriculture Insurance Consortium (TAIC), imewataka wakulima na wafugaji nchini kutumia huduma za bima ya kilimo na mifugo ili kujikinga dhidi ya hasara zinazoweza kusababishwa na majanga mbalimbali yanayoathiri uzalishaji.
Akizungumza katika Maonesho ya 33 ya Wakulima Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Dk.John Malecela Nzuguni jijini Dodoma,Mwakilishi wa TAIC, Epimack Kobero, alisema umoja huo umeundwa na kampuni 15 za bima zilizoungana kwa pamoja kutoa huduma za bima ya kilimo kwa lengo la kuimarisha ulinzi kwa wakulima na wafugaji.
Kobero alisema awali kampuni za bima zilikuwa zikitoa huduma hiyo kila moja kwa upande wake ambapo kutokana na kuongezeka kwa majanga yanayoikumba sekta ya kilimo, ikaonekana kuna umuhimu wa kuungana ili kuongeza uwezo wa kukabiliana na changamoto hizo kwa pamoja.
Alisema ushiriki wa TAIC katika Maonesho ya Nanenane unalenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa bima ya kilimo na mifugo pamoja na kuwasaidia kuelewa namna wanavyoweza kulinda uwekezaji wao.
Alieleza kuwa bima ya kilimo ni kinga muhimu inayosaidia kuongeza uthabiti wa uzalishaji kwa wakulima na wafugaji, kwani inatoa msaada pale wanapokumbwa na hasara kutokana na majanga mbalimbali.
“Kauli mbiu yetu ni kwamba kinga ya mazao na mifugo huongeza uthabiti na uzalishaji. Tunatoa elimu ili wakulima wajue umuhimu wa kulinda shughuli zao kupitia bima,” alisema Kobero.
Alifafanua kuwa changamoto kama mvua nyingi, ukame, mafuriko na magonjwa ya mifugo zinaweza kuathiri uzalishaji, hivyo bima husaidia kupunguza athari za hasara hizo na kumwezesha mkulima au mfugaji kuendelea na shughuli zake.
Kobero alisema kwa upande wa mifugo, bima inaweza kusaidia pale mifugo inapopata magonjwa au kufariki, hali ambayo inaweza kusababisha hasara kubwa kwa mfugaji.
Kobero aliwataka wakulima na wafugaji kutumia fursa ya elimu inayotolewa na TAIC pamoja na kampuni za bima ili kupata uelewa zaidi kuhusu huduma hizo na namna zinavyoweza kuwa kinga ya uwekezaji wao.

0 Comments