ADEM: WAKUU WA SHULE KUPATA MAFUNZO YA UONGOZI

 

Na Asha Mwakyonde, Dodooma

WAKALA wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) inatarajia kutoa Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Shule kwa Walimu Wakuu wapatao 17,000 .

Hayo ameyasema leo November 15,2022 jijini Dodoma Mtendaji Mkuu wa Wakala huo wa ADEM, Dk.Siston Mgullah,
wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya wakala huo na vipaumbele vyake kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Ameeleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2021/2022 wakala  huo umeweza kushirikiana na mashirika mengine katika kutoa mafunzo ya uongozi , usimamizi na udhibiti ubora wa elimu ikiwemo UNICEF, EQUIP-TZ, World Bank, GPE-LANES, PS3+, Good Neighbors (TZ, Zanzibar Office), Mwanamke Initiatives Foundation (MIF), Aga Khan University (AKU, IED, EA) na Shule Bora"amesemA.

Mtendaji huyo amesema kuwa watatoa mafunzo ya Utawala Bora kwa wasimamizi wa elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Amesema katika kipindi cha mwaka 2020/2021, Wakala umefanya tafiti mbalimbali zikiwemo za tathimini ya matokeo ya Mafunzo ya KKK kwa Walimu wa Darasa la III na IV yaliyofanyika Tanzania Bara, utekelezaji wa uthibiti ubora wa shule na utoaji wa mrejesho kwa walimu ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji katika shule za Msingi.

Aidha ameongeza kuwa Wakala umeendesha mafunzo ya Kamati za Shule kwa washiriki 126 katika Mkoa wa Songwe ili kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji katika Shule na umeandaa mtaala wa shahada ya menejimenti ya uthibiti ubora wa elimu ili kuimarisha usimamizi na utoaji wa elimu bora katika ngazi zote za elimu.

"Tumefanya tafiti sita na kuwasilishwa kwa wadau mbalimbali wa elimu ili kubaini mapungufu na kuandaa mafunzo wezeshi kwa wahusika"amesema Mtendaji huyo.

Lakini pia Wakala umeandaa Moduli 3 katika eneo la Uongozi na Usimamizi wa Shule ili kuendesha mafunzo ya kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa ujenzi wa umahiri kwa walimu wa Shule za Sekondari Zanzibar na umeandika vitabu vya kujenga umahiri katika utekelezaji wa Mtaala wa Sekondari ili kuboresha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza kwa ajili ya Shule za Zanzibar.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesema Serikali inaweka fedha nyingi kwenye sekta ya elimu nchi nzima ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23, sekta ya elimu pekee imetengewa Shilingi trilioni 5.8.

"Fedha hizi ni nyingi ambazo zinahitaji usimamizi wa karibu, hivyo wale viongozi wa kwenye taasisi zinazosimamia elimu lazima wawe na ujuzi na mbinu nzuri za kusimamia maendeleo ya elimu ili tuweze kupata thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali"amesema.

Hata hivyo Msigwa amesema Viongozi wanaosimamia Taasisi za Elimu wanatakiwa wakasome katika chuo hicho ili wakapate ujuzi wakasimamie vizuri taasisi hizo.

Post a Comment

0 Comments

 KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YANOLEWA