DK.SHEKALAGHE: UWEPO WA VYOO BORA UMEONGEZEKA NCHINI


Naibu katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk.Seif Shekalaghe ,Akizungumza  Novemba 19,2022 Jijini Dodoma, wakati wa kilele cha Wiki ya Usafi wa Mazingira Kitaifa na Siku ya Matumizi  choo Duniani,  sambamba na utoaji wa tuzo za Afya na Usafi wa Mazingira. 

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Njombe Valentino Hongoli (Kushoto), akiwa na timu yake  katika picha ya pamoja wakifurahia mfano  wa hundi ya tuzo ya ushindi wa usafi na mazingira  kundi la Halmashauri za Wilaya.

Baadhi ya viongozi mbalimbali wakifurahia jambo alilozungumza Naibu katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk.Seif Shekalaghe (hayupo pichani) Novemba 19,2022 Jijini Dodoma, wakati wa kilele cha Wiki ya Usafi wa Mazingira Kitaifa na Siku ya Matumizi  choo Duniani,  sambamba na utoaji wa tuzo za Afya na Usafi wa Mazingira.

Na Asha Mwakyonde, Dodooma

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk. Seif Shekalaghe ameeleza kuwa uwepo wa vyoo bora katika ngazi ya kaya umeongezeka kutoka asilimia 19.5 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 72.6 mwaka 2022. 

Hayo ameyasema jijjni Dodooma Novemba 19, 2022 wakati akizungumza katika kilele cha Wiki ya Usafi wa Mazingira Kitaifa na Siku ya Matumizi wa Choo Duniani, amesema uwepo wa vyoo hivyo kwa upande wa kaya umeongezeka katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Amesema Kaya zisizokuwa na vyoo kabisa zimepungua kutoka asilimia 20.5 hadi kufikia asilimia 1.4 na kwamba ujenzi wa vyoo bora pamoja na uwepo wa huduma za maji safi na salama umeongezeka katika taasisi zikiwamo  mfano shule za msingi na vituo vya kutolea huduma za afya. 

"Uwepo na matumizi ya vyoo bora ni kipimo cha ustaarabu. Kwa upande mwingine, usafi wa mazingira kwa ujumla wake unachangia  sehemu kubwa kuzuia magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza," amesema. 

Amefafanua kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita takriban shule za msingi 2,500 zimejengewa vyoo bora pamoja na vituo vya kutolea huduma za Afya vipatavyo 1,500 vimeboreshewa huduma ya maji, vyoo na sehemu za kunawa mikono. 

 "Ufuatiliaji uliofanywa na Wizara mwaka huu unaonesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita zaidi ya vituo vya njiani (Bus Stops) 280 vimejengwa na serikali pamoja na sekta binafsi ambapo huduma ya vyoo bora inapatikana wakati wa safari. Maeneo haya ni pamoja na mizani, vituo vya kuuzia mafuta, hoteli na migahawa," amesema Dk.Shekalaghe.

Dk.Shekalaghe ameeleza kuwa  Serikali itaendelea kusimamia utoaji wa huduma bora katika vituo hivi vile vile kuhamasisha uwekezaji hususani kupitia sekta binafsi ili maeneo mengi zaidi yaweze kutoa huduma kwa wasafiri na wasafirishaji katika kiwango cha ubora. 

Ameongeza kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeunda Kitengo katika Halmashauri zote kusimamia suala la Udhibiti wa Taka na Usafi ambapo kitengo hicho kina jukumu la kusimamia shughuli zote za usafi wa mazingira katika Halmashauri. 

Kwa mujibu wa Dk.Shekalaghe, Wizara ya Afya kupitia vitengo hivyo imebeba jukumu la kutoa Miongozo ya Kisera kwenye Kitengo hiki ili kiweze kutekeleza vema majukumu yake kwani madhara ya uchafu huigusa sekta ya afya zaidi pengine kuliko sekta nyingine yoyote. 

Amesema mbali na hatua hiyo Wizara ya Afya imekuwa ikisimamia uendeshaji wa Mashindano ya Afya na Usafi wa Mazingira kwa lengo la kudumisha tabia ya kupenda Usafi kote nchini ambapo kwa upande   wa Halmashauri Mshindi wa Kwanza ni Halmashauri ya Wilaya ya Njombe iliyopata asilimia 97.8%.

Kwa upende wa Kuundi la Halmashauri za Manispaa Mshindi wa Pili ni Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ambayo imepata asilimia 85.

Naye  Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Afya Mazingira Anyikite Mwakitalima,
amesema Ripoti ya Benki ya Dunia inaeleza kwamba wanapowekeza shilingi moja kwenye usafi wa mazingira wanaokoa shilingi tisa (9) ambazo zingetumika kwa namna yeyote kugharamia madhara ambayo yangetokana na uchafu ikiwemo gharama za kutibu magonjwa, muda wa uzalishaji unaopotea, vifo vya mapema na athari nyingine.

"Dhima ya Wizara ni kuhakikisha afya bora kwa kila mwananchi inatimia, hakuna chaguo jingine zaidi ya kuwekeza nguvu na rasilimali za kutosha kwenye eneo la Kinga hususani Afya Mazingira,"ameeleza.


Post a Comment

0 Comments

 KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YANOLEWA