TICD KUONGEZA PROGRAM SITA ZA MAFUNZO

 

Na Asha Mwakyonde, Dodooma

TAASISI ya Maendeleo ya Jamii Tengeru(TICD), kwa mwaka wa 2022/2023, inatarajia kuongeza program 6 za mafunzo zinazotarajiwa kuanza kutolewa dirisha la Machi 2023, maandalizi ya program hizo yamezingatia mahitaji ya soko la ajira kwa sasa ikiwa ni pamoja na kuandaa wahitimu wenye fikra sahihi na uwezo wa kujiajiri. 

Akizungumza jiijini hapa  Novemba 4,2022 Mkuu wa taasisi hiyo Dk.Bakari George wakati akitoa taasisi ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka 2022/2023 amesema matarajio yao kwa mwaka huo ni kufungua Tawi katika Mkoa wa Iringa, Wilaya ya Mafinga katika eneo la Rungemba. 

Mkuu huyo ameeleza kuwa mwaka wa masomo 2021/2022, Taasisi ilikuwa na jumla ya wanafunzi 2,747 kati ya hao, wanafunzi 1812 ni wanawake na wanafunzi 935 wanaume na kwamba idadi hiyo ni ongezeko la wanafunzi 139 ambayo ni asilimia 5.3 ya idadi ya wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2020/2021. 

"Mwelekeo unaonesha kuwa kwa mwaka 2022/2023, Taasisi itadahili jumla ya wanafunzi wapatao 3,948 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya  asilimia 43 ya wanafunzi kwa mwaka 2021/2022," Ameeleza.

Ameongeza kuwa ongezeko la udahili linachagizwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika uimarishaji wa elimu kwa ngazi za msingi na sekondari na umuhimu wa fani ya maendeleo ya jamii katika muktadha wa upatikanaji wa ajira na mawanda mapana ya kuwezesha wanafunzi kukabiliana na changamoto za soko la ajira. 

George amebainisha kuwa Serikali imefanya jitihada kubwa za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika Taasisi hiyo na kwamba sababu nyingine ya kuongezeka kwa idadi hiyo  ni upatikanaji wa mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) ambapo kwa mwaka 2021/2022, wanafunzi 448 walipata mkopo wa jumla ya Shilingi 1,153,376,000.00 na kwa mwaka 2022/2023.

Amesema idai  ya wanufaika wa mikopo inatarajiwa kuwa takribani wanafunzi 450 watakaopata jumla ya Shilingi 1,158,525,000.00 na kwamba  katika kipindi cha miaka mitano (2015/2016 hadi 2020/2021), Taasisi imetoa jumla ya wahitimu 2,350 ambao baadhi yao wameajiriwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Mashirika yasiyo ya kiserikali na wengine kujiajiri wenyewe. 

Mkuu huyo wa chuo amesema kwa mwaka 2020/2021, jumla ya wanafunzi 1,455 walihitimu ambapo kati ya wahitimu wote, 15 walitunukiwa Shahada ya Uzamili 242 walitunukiwa Shahada ya Kwanza, 235 walitunukiwa Stashahada, 370 walitunukiwa Astashahada na wengine 613 walitunukiwa Astashahada ya Msingi. 

"Tunamshukuru Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kufungua milango ya ajira ambazo zimewezesha baadhi ya wahitimu wetu kuajiriwa kama Maafisa Maendeleo ya Jamii, Wahadhiri, Watendaji wa Kata na Vijiji, Maafisa Mikopo na wengine wameajiriwa kwenye vyombo mbalimbali ya ulinzi na usalama," amesema. 

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI