TALAKA, KUTENGANA KUNAVYOATHIRI MAKUZI YA MTOTO KATIKA LISHE


 NA ASHA MWAKYONDE, DODOMA

UTAFITI uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), wa kufuatilia kaya hapa nchini Tanzania wa mwaka 2014/ 2015 umeonesha kiwango cha talaka kimeongezeka kwa asilimia 1.1.

Hali hii imesababisha ongezeko la watoto wa mitaani kwa kukosa makuzi, malezi bora ikiwemo masuala ya lishe.

Mtoto, watoto kulelewa upande mmoja wa baba au mama kuna athari ambazo zinaweza kujitokeza ikiwa ni pamoja na kujiingiza kwenye makundi yasiyofaa, kufanyiwa vitendo vya ukatili, kubakwa au kulawitiwa.

Kuna athari katika makuzi ya mtoto kukosa lishe bora mfano mama asiye na kipato cha uhakika hawezi kumudu gharama za utafutaji wa chakula, hivyo mtoto hatapata lishe nzuri na kwa wakati.

Hali hiyo itasababisha mtoto kwenda mitaani kujitafutia chakula na inaweza kuwa kwa kuomba omba au hata kujiingiza katika makundi yasiyofaa na kusababisha kuwapo kwa watoto wanaojiita panya rodi.

 VIONGOZI WA DINI WANENA

Wakizungumzia suala la kutengana, kutalikiana kwa wazazi, viongozi wa dini wamesema wana nafasi kubwa ya kusuluhisha ndoa walizozisimamia na kuzifungisha ili kuepuka athari zitakazojitokeza kwa watoto pindi wana ndoa watakapotengana.

Sheikhe wa Mkoa wa Dodoma, Alhaji Mustapha Rajabu ameeleza kuwa nafasi ya viongozi wa dini ni kubwa katika kutoa suluhu ya masuala ya ndoa kwa kuwa ndipo ndoa hizo zinapofungiwa hivyo, wanajukumu la kusimamia migororo inapotokea ya ndoa, talaka na hata mirathi.

“Watu wote wapo chini ya viongozi wa dini kama hatakuwa muislamu atakuwa mkristo, na hapa Tanzania kuna dini mbili ambazo ni kubwa ya Kiislamu na Kikiristo hizo nyingine ni madhehebu.

Bila viongozi wa dini hawataitwa wanandoa, wanaitwa wanandoa kwa sababu viongozi wa dini wamewasimamia na kama tunawasimamia katika ndoa hata nafasi ya kusuluhisha migororo yao inakuwa ni kubwa kuliko sehemu nyingine yoyote," amesema.

Ameeleza kuwa watoto wanapatikana baada ya viongozi wa dini kusimamia ndoa kati ya mume na mke hivyo malezi bora ya watoto yanaanzia nyumbani kwa yule aliyeozeshwa na viongozi hao.

Kiongozi huyo wa dini ameongeza kuwa baba na mama wanajukumu la kuhakikisha wanawasimamia watoto wao waende madrasa kusoma dini, kuabudu misikitini au makanisani kwani ni jukumu ambalo linatakiwa kufanywa na wazazi wote wawili.

Alhaji Rajabu amefafanua kuwa wazazi wengi wanashindwa kutofautisha kati ya kulea na kufuga huku akisema kulea ni kumlea kijana katika maadili na kumfuga ni kumtimizia mahitaji yake yote lakini hana adabu, heshima na ucha Mungu.

“Wazazi wanapoachana wanamuweka mtoto njia panda anakuwa haelewi aende kwa baba au mama na kila mmoja anataka kuonyesha mapenzi kwa mtoto ndipo wanapofuata matakwa ya mtoto huyo.

Kwa kutokuwa na maadili sahihi mzazi anaonekana hakumlea mtoto wake bali alimfuga maana hata mbuzi, ngo'ombe, kondoo na kuku hufugwa na wanapewa maji, wanapekekwa kuchungwa na wanapewa kila huduma,”amesema

Mtoto anayeishi katika mazingira ya wazazi waliotengana huyo ni nusu ya yatima kwa kuwa hatekelezewi, halelewi katika malezi chini ya wazazi walio pamoja katika maisha ya ndoa.

Naye Askofu wa Kanisa la Christian Mission Fellowship Tanzania Donard Mhango amesema wao kama viongozi wa dini wanafasi ya kutoa ushauri kulingana na namna ndoa ilivyofingwa au ilivyounganishwa.

Askofu huyo amebainisha kuwa kuna ndoa nyinyi za kimila, kiserikali na za kidini inategemea na hiyo migororo ya ndoa ipo katika eneo gani kati ya ndoa hizo tatu na kwamba mara nyingi wanapenda kutoa ushauri hata zile zinazoendena na za kidini.

Kwa mujubu wa Askofu huyo ndoa za kidini zinaongozwa na vitabu ambavyo ni vya Quran na Biblia hivyo waliofunga ndoa wanapaswa kufuata taratibu na kanuni zilizopo kwenye mpango wa Mungu kama alivyoagiza.

Kutokana na aina hiyo ya ndoa amesema inawapa fursa ya kushauri wanandoa kulingana na migogoro yao wanaangalia kanuni na taratibu zake.

"Kwa upande wetu sisi wakristo ndoa zimeshawekwa katika mpango wa Biblia mwanamke na mwanaume wanapokubali kuwa mke na mume hata kama ingetokea mgongoro wa aina gani ndoa hiyo inahitaji uvumilivu, Biblia inasema ndoa anayoiunganisha ni Mungu sio mwanadamu na hakuna anayeweza kuitenganisha labda Mungu mwenyewe, ndoa ya kikristo hairuhusiwi kuachana," amesema.

Askofu huyo akizungumzia umuhimu wa malezi ya watoto amesema ni ya baba na mama hivyo wanawahimiza wazazi wote kulea watoto wao kwa kushirikiana.

Ameongeza kuwa pindi wazazi hao wanapokuwa na migogoro au wanapotengana wahanga wakubwa wanakuwa ni watoto hivyo kinachohitaji ni kusameheana huku akisema kuwa wao kama viongozi wa dini muda mwingine wanatumia ushawishi wa kibinadamu ili wasitengane, wasiachane.

MAONI VIONGOZI WA DINI

Viongozi hao wameeleza kwamba ili kutengeneza jamii iliyobora na salama lazima kuhakikisha vijana wanahofu ya Mungu, wasipokuwa na hofu hiyo Taifa linapata vijana waliokosa malezi bora, vibaka, wezi, watumia unga, madawa ya kulevya, wavuta bangi na walevi ni kutokana na kutokua katika maadili sahihi.

 Wamesema migororo ya wazazi isiwasababishie watoto kuwa wahanga kama wazazi hao watakuwa na changamoto zao suala la malezi ya watoto libaki pale pale.

Wazazi wajitahidi kuvumiliana katika ndoa zao,kusikilizana na kuheshimiana Ili ndoa hizo zidumu zinapodumu watoto watalelewa na kukuzwa katika makuzi yaliyobora.

 MZAZI ANAYELEA WATOTO PEKE YAKE

Mkazi wa Nkuhungu jijini Dodoma, Eva Fumbe anayelea watoto wake watatu, wa kiume wawili na wakike mmoja amesema kuna changamoto nyingi za kulea familia katika upande mmoja ikiwamo kushindwa kumudu baadhi ya mahitaji kama vile lishe.

Eva ameeleza kuwa anajitahidi kadri ya uwezo wake lakini hali ya maisha kwake imekuwa ni ngumu hata muda mwingine kukosa chakula.

"Kutokana na hali ngumu ya maisha niliyonayo hata mwanangu wa kwanza amemaliza kidato cha nne mwaka jana na kupata ufaulu wa alama 3. 22 lakini hakupata nafasi serikalini ananiumiza kichwa ningekuwa na hela ningempeleka shule binafisi," amesema.

Amesema kuwa tangu aachane na mume wake mwaka 2007, anaendelea kupambanana mwenyewe kuhakikisha watoto wake wanapata mahitaji japo hayajitoshelezi.

Eva ni mjasiriamali wa kutengeneza sabuni za maji, batiki na mafuta ya mgando amesema mtaji wake haukui kutokanana na kidogo anachokipata ananunua mahitaji ya familia yake.

Ameongeza kuwa anatamani ndoto zake za kumiliki kiwanda zitimie lakini kikwazo kikubwa ni kutokuwa na mtaji wa kujitosheleza.

MTOTO ALIYELELEWA NA MZAZI MMOJA

Haruna Mwenda ni mkazi wa Ilazo ambaye amelelewa upande mmoja wa baba baada ya wazazi wake kutengana na kwa sasa ni baba wa watoto wawili amesema malezi ya kulelewa na wazazi wote wawili yanamfanya mtoto kuwa huru na kujiamini.

Mwenda amesema mtoto anayelelewa na mzazi mmoja kuna baadhi ya vitu huvikosa ikiwemo lishe bora pamoja na malezi ya wazazi wote wawili.

Akizungumzia athari Mwenda amefafanua kuwa ni pamoja na  kunyanyaswa..

"Kwa upande wa manyanyaso mtoto anayelelewa na mzazi mmoja anaweza kuathirika kisaikolojia kutokana na kutumia muda mwingi kumuwaza mzazi wake wa pili pindi anapoona hajatendewa haki," ameongeza

"Nililelewa na mzazi mmoja ambaye ni baba, alioa mke mwingine, mama wa kambo hakuwahi kunipenda. Kila siku nashtakiwa kwa baba hata kama sijafanya kosa na alikuwa na mtoto wake, chakula alikuwa anampendelea," ameeleza.

Kuna baadhi ya mazingira yanamlazimu mtoto kupata malezi ya pande mbili tofauti na wazazi wao nayo pia sio mazingira mazuri katika makuzi ya mtoto lakini yapo mazingira ya wazazi kutengana na kusababisha mtoto kulelewa na mzazi mmoja," amesema Mwenda.

Akizungumzia faraja za watoto hao Mwenda amebainisha kuwa zinatofautiana huku akitolea mfano mtoto anayelelewa na mama hamjui baba alipo na huwa anajifariji kwamba akikua atamtafuta.

 SUALA LA LISHE

Akizungumzia umuhimu wa lishe kwa mtoto, Afisa Lishe kutoka Wizara ya Afya Kitengo cha Huduma za Lishe Jenipha Mayenga amesema kuwa katika ukuaji wa mtoto na uwezo, lishe bora huwapa watoto nishati ya kuishi maisha kamili, huwalinda dhidi ya utapiamlo, kudumisha mfumo wa kinga, kuzuia unene na kupunguza hatari ya magonjwa sugu.

Kwa upande mwingine Afisa huyo ameeleza kuwa lishe duni hasa katika siku 1,000 za kwanza za maisha ya mtoto (kuanzia kipindi cha ujauzito hadi mtoto anapofikisha umri wa miaka miwili) inaweza kusababisha matatizo ambayo hayawezi kurekebishika kama kumuweka katika hatari ya udumavu wa mwili na ubongo ambayo huweza kuathiri uwezo wa kufanya vizuri shuleni.

Ameongeza kuwa watoto waliodumaa huwa na uwezo mdogo wa kushiriki na kuhusiana na watoto wengine vizuri katika michezo na maeneo mengine.

"Lishe duni husababisha kuwa na kinga duni dhidi ya magonjwa hivyo humfanya mtoto augue mara kwa mara, pia lishe duni kwa watoto inawaweka katika hatari ya kupata unene wa kupindukia baadaye, kisukari, na magonjwa mengine sugu ambayo yanaweza kusababisha matatizo ya kiafya maishani," amesema.

Afisa huyo amewashauri wazazi kuhudhuria kliniki na endapo mtoto atapata changamoto katika makuzi yake na ulaji kama kutoongezeka uzito, mtoto kukataa kula baadhi ya vyakula ni vyema mzazi apate ushauri kutoka kwa watoa huduma wa afya waliopo katika vituo vya afya nchini.

SHERIA YA MTOTO

Akizungumzia sheria inamlinda vipi mtoto katika makuzi yake, Mwanasheria ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema Sheria ya mtoto ya mwaka 2009 kama inavofanyiwa marejeo ya mara kwa mara pamoja na sheria nyingine kuna mambo mawili maalum yanayomlinda mtoto  kupata haki ya makuzi ambazo  ni sheria ya ndoa ( The law of Marriage Act) na Sheria ya Mtoto (The Law of the Child Act).

Mwanasheria huyo ameeleza wa mujibu wa kifungu namba 8 na 9 cha sheria ya mtoto kinaelekeza wajibu wa wazazi, walezi kumtunza mtoto kwa kumpatia chakula, Mavazi, Makazi na matibabu ikiwa ni pamoja na kumpatia chanjo, elimu na malezi.

“Mtoto apatiwe uhuru na haki ya kucheza, kupumzika kwa lengo la kuhakikisha makuzi bora kwa mtoto,”amesema Mwanasheia huyo.

 MWANASAIKOLOJIA

Askofu wa Kanisa la Pentekoste Tumaini Gospel Centre nchini Tanzania Profesa Rejoice Ndalima ambaye pia ni mwanasaikolojia amesema mtoto anapokutana na wenzake wanaolelewa na wazazi wote wawili wanapohadithiana upendo wanaoupata kwa wazazi wao, kwake haupo inamuathri kisaikolojia kwa kujiona upendo huo haupati.

Mwanasaikolojia huyo amefafanua kwa mtoto huyo atakapokuwa mtu mzima anakuwa mkali mkali bila sababu, kutojiamini, kuwa na tabia za ajabu ajabu.

Amesema zipo athari zitakazomwathiri mtoto kisaikolojia kama hajalelewa na wazazi wawili hatakuwa anajiamini, hana furaha muda mwingine kujisikia mnyonge, kukosa mahitaji ya lazima na ushauri wa msingi.

USHAURI

Anasema kuwa ni vema wazazi wanaowalea watoto pekee yao bila mzazi mwenzake wanatakiwa kuwakutanisha watoto wao na ndugu zao wa karibu kama wajomba, mama wadogo yaani wale watu wa karibu ili kupata faraja ya maneno ambayo anayakosa kwa mzazi mwingine.

“Wazazi wengi hawajui wanafikiri kumnunulia sare za shule, kumlipia ada, kumpata chakula, malazi ndio ndio malezi, kumjenga kisaikolojia inamwandaa awe nani baadae,”amesema Mwanasaikolojia huyo. 

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI