TASAC YAKANUSHA NA KUFAFANUA TAARIFA ZINAZO SAMBAA MITANDAONI


 Na Asha Mwakyonde,Dodoma

SHIRIKA la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) limekanusha Taarifa zilizokua zikisambaa hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii  kuhusu Mikataba ya mafunzo kazi kwa vijana zaidi ya 400 waliokuwa TASAC ilivunjwa bila kufuata utaratibu na ikiwa imebaki muda wa mwaka mmoja kuisha kwa mikataba hiyo.

Akizungumza Jijin Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC,Kaimu Mkeyenge amesema  hivi karibuni kumekuwa na taarifa zikisambaa katika mitandao ya kijamii ya ikiwamo Instagram na Twitter amesema taarifa  hiyo ilieleza kuwa vijana hao walifanya kazi bila bima ya afya na kwamba shirika  hilo ilitoa rushwa kwa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) katika mashauri ya kazi yaliyofunguliwa na vijana hao ili haki isitendeke.

"Mnamo mwezi Julai, 2022 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilifanya mabadiliko ya Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania kwa kufuta majukumu ya kipekee ya uwakala wa meli, uhakiki wa mizigo, udhibiti wa nyaraka na kupunguza wigo wa jukumu la kufanya uwakala wa forodha katika bidhaa zilizokuwa zinagombolewa na kuondoshwa na TASAC.
 
TASAC ilikuwa ikitekeleza majukumu hayo kupitia vijana waliokua wameajiriwa moja kwa moja pamoja na waliokuwa wakifanya mafunzo ya kazi lakini kufuatia mabadiliko hayo, Agosti 11, 2022 TASAC ilivunja mikataba ya mafunzo ya kazi kwa jumla ya vijana 209 waliokuwa wakifanya kazi za uhakiki wa shehena na si zaidi ya 400 kama ilivyoripotiwa katika mitandao ya kijamii." Amesema Mkeyenge 

Hata hivyo amesema Vijana hao waliandikiwa barua kuwa mikataba yao haitahuishwa tena ifikapo tarehe 30 Agosti, 2022 kutokana na merekebisho ya Sheria ambayo yamesababisha baadhi ya majukumu ya TASAC kufutwa na kuhamia sekta binafsi.
 
"Kwa mujibu wa masharti ya mikataba, TASAC ilikuwa inawapa mkataba ya miezi mitatu na kuongeza muda kila ilipoonekana inafaa kutokana na utendaji kazi wa mtu"amesema Mkeyenge. 

Aidha, mikataba ilikuwa imeainisha utaratibu wa namna ya kuvunja mikataba ya mafunzo kazi na ndio utaratibu uliotumika kuvunja mikataba hiyo.

Kwa kuwa vijana wanaolalamika walikuwa kwenye mafunzo kazi na sio waajiriwa wa moja kwa moja, TASAC kama taasisi nyingine yoyote ya Serikali haina wajibu wa kuwakatia bima ya afya vijana inaowachukua kwa mafunzo kazi kwani stahiki zao zimeainishwa kwenye Muongozo wa Kitaifa wa Mafunzo Kazi uliotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu.

Amesema , TASAC ni taasisi ya Serikali inayosimamiwa na Sheria, Kanuni na Miongozo ya Serikali, hivyo  mashauri yake kisheria yanasimamiwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ikiwa ni pamoja na shauri hilo na kuwahakikishia shirika hilo halijatoa na haiwezi kutoa rushwa yoyote kwa CMA ili kuzuia haki isitendeke kama ilivyoripotiwa katika mitandao ya kijamii.

"Ningependa mfahamu ya kuwa, kati ya vijana 209 waliofutiwa mikataba yao, ni vijana 41 tu ambao hawakuridhika na maamuzi hayo. Vijana 32 kati ya vijana 41, shauri lao lilifutwa na CMA kwa kuwa liliwasilishwa nje ya muda, hivyo ni vijana 9 tu ambao shauri lao dhidi ya TASAC lilipokelewa na lipo katika Tume ya Usuluhisi na Uamuzi vijana 168 waliobaki hawakupinga uamuzi wa TASAC wa kuvunja mikataba yao kutokana na mabadiliko ya Sheria ambayo yalikuwa ni nje ya uwezo wa Shirika."amesema Mkeyenge 

Amesema kwa kuwa suala hilo lipo kwenye chombo cha maamuzi kisheria, TASAC haipaswi kulizungumzia shauri hilo lakini ilionekana ni busara kulitolea ufafanuzi wa kilichofanyika kwa upande wa TASAC na kuacha hatua za maamuzi zinazoendelea kuchukua mkondo wake.

TASAC kama Shirika la Umma linatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayotolewa na Serikali, hivyo linatoa wito kwa Umma kuwa na subira wakati Tume inapoyafanyia kazi mashauri hayo.


Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI