WANAOTUMIA MITANDAO YA KIJAMII KUDHALILISHA WALIOFANYIWA UKATILI WAONYWA

Na WMJJWM, Dodoma

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa onyo kwa wote wanaotumia mitandao ya kijamii kuweka picha na maudhui ya kudhalilisha waathirika wa vitendo vya ukatili.

Waziri Dkt. Gwajima ametoa onyo hilo kwenye Mkutano wa 12 kikao cha kwanza Bungeni leo Agosti 30, 2023 alipokuwa akijibu swali la Mhe. Fatma Toufiq aliyetaka kauli ya Serikali kuhusu watu wanaowapiga picha waathirika wa ukatili na kuzirusha mtandaoni.

"Kwa sababu hawasikii niseme sasa hili ni onyo la mwisho, vinginevyo nitaitisha kikao cha wadau wote na mimi mwenyewe kuongoza kuwashitaki kwa mujibu wa Sheria" amesema Waziri Dkt.Gwajima.

Kuhusu mpango wa Serikali wa kujenga nyumba salama kwa waathirika wa ukatili nchini, lililoulizwa na Mhe. Martha Gwau, Waziri Gwajima amesema Serikali imeandaa mwongozo wa uanzishaji na uendeshaji wa nyumba salama wa mwaka 2019 kwa ajili ya manusura wa vitendo vya ukatili na wahanga wa biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu.

Amesema lengo la uanzishaji wa Mwongozo huo ni kuweka mazingira wezeshi ya uanzishaji wa huduma ya nyumba salama kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia na kwa watoto.

"Hadi kufikia mwezi Juni 2023, tayari nyumba salama 12 zimeanzishwa na kusajiliwa katika mikoa ya Dar Es Salaam, Kigoma, Arusha, Mwanza na Kilimanjaro" amesema Waziri Dkt. Gwajima.

Aidha, Dkt. Gwajima ameziomba Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na wadau wa maeneo yao, kutumia mwongozo huo kuanzisha nyumba hizo wakati Wizara ikiendelea kutafuta rasilimali fedha ili kuongeza nguvu.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU