WANAOISHI MABONDENI WATAHADHARISHWA MVUA ZA EL-NINO


Na Asha Mwakyonde, Dodoma

WANANCHI wanaoishi na kuendesha shughuli za kiuchumi maeneo ya uwanda wa chini na pembezoni mwa mabonde ya maji wanatahadharishwa kuchukua hatua ili kunusuru maisha na mali zao.

Hivi karibuni Mamlaka ya Hali ya Hewa  Tanzania (TMA), ilitoa utabiri wa mwelekeo wa mvua za vuli  kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2023 ambapo utabiri huo umeonesha uwepo wa El- Nino itakayosababisha vipindi vya mvua kubwa ambazo zitaendelea hadi Januari 2024.

Akizungumza leo Agosti 31,2023  jijini Dodoma Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama alisema kuwa madhara yanaweza kujitokeza kuipitia uwepo wa mvua hiyo mvua  El-Nino.

Aidha ametoa wito kwa Umma kutumia mvua hizo ili ziwe na manufaa kupitia shughuli za uzalishaji mali kama kilimo, kuandaa mabwawa  na malambo kwa ajili ya kuvuna maji, kupanda mazao yanayohitaji maji mengi yakiwamo mpunga, uzalishaji wa samaki na kuhifadhi malisho  ya mifugo.


Kutokana na mvua hizo zinazotarajiwa kuwa na madhara Waziri huyo amezielekeza Kamati za Usimamizi wa Maafa za mikoa, Wilaya, Kata na vijiji au Mita kuchukua hatua lengo likiwa ni kuzuia na kupunzuza madhara  ya majanga na kujiandaa kukabili na kurejesha hali endapo maafa hayo yatatokea kwa kuzingatia sheria ya Usimamizi wa Maafa namba 6 ya mwaka 2022 na kanuni zake.

" Serikali inaelekeza kamati hizi za usimamizi wa maafa na sekta kushirikiana na Umma kuchukua hatua juu ya madhara hayo," amesema Waziri huyo.

Aidha Waziri Mhagama amezitaja hatua zitakazo chukuliwa na kamati hizo  kuwa ni kutambua maeneo hatarishi na yenye viashiria vya kuathirika na maafa na kuandaa mipango ya kuzuia madhara na kukabiliana na maafa hayo endapo yatatokea, kuainisha na kuandaa rasilimali za usimamizi wa maafa kwa kila sekta kushiriki kikamilifu katika eneo lake.

Waziri Mhagama amesema  hatua nyingine ni kuandaa mipango ya kuzuia milipuko ya magonjwa kwa binadamu, wanyama na mimea, kuhifadhi mazingira na kulinda miundombinu ya barabara, maji,Umeme na mawasiliano ili kupatikana huduma wakati wote.

Ameongeza kuwa hatua hizo ni pamoja na kuelimisha wananchi juu ya hatua za kuchukua tahadhari ili kuokoa maisha na mali, kutoa taarifa kwa haraka kwa Mamlaka husika dalili za kutokea maafa hayo yanapaotokea, kuhama kwenye maeneo hatarishi na kutekeleza shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo salama.


MADHARA YA MVUA ZA EL-NINO

Waziri Mhagama ameyataja madhara yatokanayo na mvua hizo kuwa ni mafuriko kuharibu miundombinu, madhara kiafya, kiuchumi, kijamii na upotevu wa mali, maporomoko ya ardhi kuathiri makazi, mazingira, mashamba, usafiri na shughuli zingine hususan uchimbaji madini.

Amesema madhara mengine ni magonjwa ya milipuko kwa binadamu na wanyama na wadudu waharibifu wa mazao na mimea.

Waziri huyo amesema  Ofisi ya waziri Mkuu itaendelea kiratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa maafa nchini kwa kuzingatia Sheria sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004, Sheria ya usimamizi ya Maafa namba 6 ya mwaka 2022  pamoja na maelekezo ya Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 hadi 2025 na mikakati, mipango na miongozo.

Msimu wa mvua za vuli ni mahususi kwa maeneo yanayopata mvua misimu miwili ya mvua kwa mwaka katika mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, kusini mwa mkoa  Simiyu , Kaskazini mwa Kigoma, Dar es salaam, Tanga, Pwani ikiwamo Visiwa vya Mafya na Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI