Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kondoa, Said Majaliwa akifafanua jambo kwa wajumbe (hawapo pichani), katika kikao ndani ofisini kwake.
Afisa Biashara Emmanuel Masey kutoka Halmashauri ya Mji Kondoa akikagua leseni katika moja ya duka la mfanyabiashara kwenye Halmashauri hiyo.
Na Asha Mwakyonde,DODOMA
HALMASHAURI ya Mji Kondoa iliyojiwekea malengo makuu kumi na moja, yakiwamo kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kufikia asilimia 100 ambapo hadi kufikia Juni, mwaka huu imefikia asilimia 99 ya mapato yote.
Akizungumzia taarifa ya utendaji kazi ya Idara ya Biashara,Viwanda na Uwekezaji kupitia baraza la madiwani la mwisho wa mwaka 2023/2024 Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Said Majaliwa anaeleza kuwa ukusanyaji wa mapato wa Halmashauri hiyo kuanzia Julai 2023 hadi Juni 2024 Idara imefanikiwa kukusanya mapato kutoka vyanzo mbalimbali ambavyo ni leseni za biashara, ambapo zaidi ya shilingi milioni 126.
Mkurugenzi huyo anafafanua kuwa fedha hizo zimekusanywa kutoka kwenye leseni za biashara ambazo ni sawa na asilimia 90.15 ya makisio ya bajeti ya Shilingi milioni 140.
Akizungumzia leseni za vileo anasema kuwa zaidi ya shilingi milioni 3.2 zimekusanywa kutoka kwenye leseni za vileo ambazo ni sawa na asilimia 81.60 ya makisio ya bajeti ya Shilingi milioni 4.
"Zaidi ya shillingi milioni 58 zimekusanywa kutoka kwenye ushuru wa nyumba za kulala wageni ambazo ni sawa na asilimia 105.69 ya makisio ya bajeti ya Shilingi milioni 55," anasema Mkurugenzi Majaliwa.
Anaongeza kuwa jumla ya Shilingi 820,000 zimekusanywa kutoka kwenye ada ya matangazo ambazo ni sawa na asilimia 82 ya makisio ya bajeti ya Shilingi 1,000,000.
MIKAKATI YA IDARA
Mkurugenzi huyo anaeleza kuwa Halmashauri hiyo imeweka mikakati mbalimbali ikiwamo ya kusimamia sheria, kanuni taratibu za uendeshaji wa biashara kwa wafanyabiashara.
"Tumetoa elimu kwa wafanyabiashara ili kufahamu umuhimu wa kuwa na leseni ya biashara, kulipa kodi na tozo mbalimbali za Serikali kwa hiari,anasema Majaliwa.
CHANGAMOTO
Akizungumzia changamoto za mfumo unaotumika katika usajili (TAUSI) kutokuwepo mara kwa mara, hivyo kushindwa kuwasajili wafanyabiashara kwa ajili ya malipo kwa wakati.
Majaliwa anaongeza kuwa changamoto nyingine ni baadhi ya wafanyabiashara kutokuwa na namba ya mlipa kodi (TIN), na namba ya uraia (NIDA).
UTATUZI WA CHANGAMOTO
Mkurugenzi huyo akizungumzia namna Halmashauri hiyo ilivyo shirikiana na ofisi ya NIDA anasema kuwa ofisi ya Mamlaka ya vitambulisho tayari imerahisisha upatikanaji kwa namba za uraia kwa wafanyabiashara.
"Tunaelea kushirikiana na ofisi za TEHAMA katika kutatua changamoto za mfumo wa TAUSI, " anaeleza Mkurugenzi huyo wa Mji Kondoa.
Anaongeza kuwa Halmashauri hiyo ina endelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara, kutoa matangazo lengo likiwa ni kuwakumbusha wafanyabiashara umuhimu wa kuwa na leseni za biashara za kulipa tozo za serikali.
0 Comments