Na Mwandishi wetu
SERIKALI imewaagiza washauri wa wanafunzi na maafisa wa huduma za wanafunzi vyuo vya elimu ya juu na kati Tanzania ( TACOGA1984) Kushirikiana na serikali katika kukemea na kupambana na vitendo vya mmomonyoko wa maadili kwa wanafunzi ili kusaidia kutunza tunu ya Taifa ya kuwa na maadili mema ya kitanzania.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa masuala yahusuyo jinsia kutoka wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Ndg. Badru Abdunuru wakati akifunga Mkutano Mkuu wa 41 wa Chama Cha washauri wa wanafunzi na maafisa wa huduma za wanafunzi vyuo vya elimu ya juu na kati Tanzania (TACOGA1984) uliofanyika Septemba 28,2023 Jijini Dodoma.
“Nyinyi naomba mtambue dhamana mliyopewa, hali kadhalika kazi mnayofanya inamchango mkubwa kwa maisha ya Watanzania, sasa niwaombe na naamini wote mnaelewa changamoto kubwa ambayo nchi tunayo kwa sasa ni mmomonyoko wa maadili na tiba au suluhisho lake ni nyinyi, na mchango mkubwa katika hili ni pamoja na kazi mnazozifanya vyuoni. Niwaombe hili nalo mlichukulie kwa uzito wake,” amesema Ndg. Abdunuru.
“Jamii tunayoiandaa vyuoni inahusu utumishi wa umma na Taasisi binafsi, kwa msingi huo tukiwa na kizazi zoofu na chenye mmomonyoko wa maadili tutakuwa na Taifa ambalo ni dhaifa pia.”.
“ Kabla hatujaelekea huko niwaombe katika hili, wote tumesikia kuanzia viongozi mbalimbali wa nchi Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla ikizungumzia na kutoa rai kwa Watanzania na jamii kwa ujumla kuhusu maadili ya kitanzania na tunu za Taifa, hivyo utendaji wenu uonyeshe kwa dhati na kwa vitendo katika hili suala la mmonyoko wa maadilli,” amefafanua Ndg. Abdunuru.
Akizungumza kwa niaba ya katibu Mkuu wa wizara ya maendeleo ya jamii , Jinsia , Wanawake na Makundi Maalum Mkurugenzi Abdunuru amesema atahakikisha anaisemea TACOGA1984 kwenye wizara yake ili kuwe na mkakati wa kujengewa uwezo kwa kupewa mafunzo maalum kwa ajili ya kuhudumia makundi maalumu, pia inahitajika elimu kuhusu dawati la jinsia.
Awali mwenyekiti wa Chama cha TACOGA1984 Bi. Sophia Nchimbi amesema mafanikio yaliyopatikana katika chama hicho ni kununua vifaa kwaajili ya kuendeleza chama, kuwepo kwa Tovuti ya chama na mahusiano mazuri na Taasisi nyingine.
Bi. Nchimbi amesema pia kuwa pamoja na kuwepo kwa mafanikio lakini bado kuna changamoto inayowakabili, nayo ni ucheleweshwaji wa ulipaji ada toka kwa wakuu wa vyuo na kuiomba serikali kupitia Wizara ya Elimu kuwahamasisha wakuu hao kulipa ada na kwa wakati.
Chama cha washauri wa wanafunzi vyuo vya elimu ya juu na kati Tanzania ( TACOGA1984) kilianza mwaka 1984 na kusajiliwa upya mwaka 2019 kikiwa na lengo la kutoa elimu na mafunzo mbalimbali kwa Wanachama na viongozi wa serikali za Wanafunzi, kutoa ushauri na unasihi kwa wanafunzi wa elimu ya juu kuhusu masuala mbalimbali kama vile, namna ya kujisomea ili kuweza kumaliza elimu yao, pia kutoa elimu kuhusu matumizi ya fedha pindi wawapo masomoni.
0 Comments