SHIRIKA LA ASPA KUJA NA MKAKATI UJENZI MABANDA YA PUNDA SOKONI


Na Asha Mwakyonde,Dodoma

PUNDA ni mnyama kazi ambaye hutumiwa zaidi na watu waliopo maeneo ya vijijini hasa wanawake, na wafanyabiashara ndogo ndogo wanaoishi katika maeneo hayo.

'kuna usemi usemao 'Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni', usemi huu  ungetumiwa vizuri kwa  mnyama Punda huenda angeheshimika zaidi kutokana na shughuli zake za kila siku katika kumsaidia mwanadamu kwenye majukumu yake.

Punda ni mnyama mpole na mvumililivu wakati wowote hata anapokuwa na mzigo mzito na akizidiwa anakaa chini  lakini hathaminiwi kwa kupatiwa mahitaji muhimu.

Kutokana na kutokuthaminiwa Shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake makuu mkoani Arusha la Arusha Society for the Protection of Animals (ASPA), ambalo lina fanya kazi ya kutetea Ustawi wa wanyama (welfare animal), na haki zao wale waliosahaulika.

Mkurugenzi wa Shirika hilo la  ASPA, Livingstone Masija ameeleza kuwa wamekuwa wakijihusisha zaidi na masuala ya  wanyama waliosahaulika kama paka, mbwa na Punda.

Akizungumzia mnyama Punda ambaye anafanya kazi ya  kumsaidia mwanadamu kumbebea mizigo hasa mwanamke  katika kikao cha siku moja cha kujadili Ustawi wa mnyama huyo  kilichofanyika hivi karibuni Jijini Dodoma  amesema mkoani Arusha wananchi wamekuwa wakimtumia mnyama huyo kubebe bidhaa mbalimbali wanazoenda kuuza sokoni kama kuni, maharage, mahindi mkaa na mazao mengine.


Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa wananchi wamekuwa na tabia ya kutowajali  Punda  waliobebe mizigo sokoni ambapo wanawafunga juani bila kuwapatia maji na chakula.

Amesema Punda wamekuwa wakifungwa juani kuanzia wanapofika sokoni hadi muda wa kuondoka jioni na wanaporudi nyumbani  wanabebeshwa bidhaa nyingine ambazo wananchi hao wamekuwa wamezinunua bila kupewa kula.

Masija ameeleza kuwa wananchi hao wanapofika nyumbani hawawakumbuki Punda kuwapatia chakula na maji huku akisema mnyama huyo amekuwa akishambuliwa na fisi.

JITIHADA ZA ASPA

Amesema kutokana na mateso hayo ya punda kama Shirika wameanza mchakato wa kujenga mabanda ya kumpumzikia Punda hao wanapofika sokoni ambapo tayari  wameshaanza  kujenga mabanda hayo  matatu katika eneo la Milongoine.

"Kila banda lina maji ya kunywa Punda na tunajitahidi kuwatafutia pumba ili wale na kupumzika na hata mwenye punda akiwafuata kwa ajili ya kurudi nyumbani tayari watakuwa wameshiba," amesema.

Ameongeza kuwa hali ni mbaya katika masoko mbalimbali yaliyopo Arusha huku akiyataja baadhi ya  masoko hayo kuwa ni soko la Kia, Kikatiti, Ngarenanyuki, Ngaranaibu.


Mkurugenzi huyo amesema wanaendelea kujenga mabanda katika masoko mbalimbali pamoja na kuyawekea maji na huduma nyingine muhimu ili waweze kufaidika na matunda ya kazi zao.

Amefafanua kwamba, kwa kuwa masoko ni mengi hapa nchini na mobile market nyingi zinazohudumiwa na Punda zipo mkoani Arusha wameona waanze na mkoa huo baadae wataendelea na mikoa yenye uhitaji.

"Kwa mfano tumekuwa tukienda Mkoa wa Geita kwenye machimbo ya dhahabu  ya Mgusu, Punda waliopo katika machimbo hayo wanaojihusisha na ubebaji wa mifuko ya michanga, tumeona mahitaji yao mengi ni matibabu kwa kuwa wanachubuka na kupata vidonda.

Ameongeza kuwa Punda waliopo Mgusu hawahitaji kujengewa mabanda kutokana na kazi yao kubwa ni ya ubebaji mifuko na kwenda kusaga michanga hiyo na kwamba Punda hao wamejengewa sehemu za maji ya kunywa ili wanavyopanda milimani wasichoke.

"Pia Punda hawa tumekuwa tukiwapatia matibabu ya dawa za  minyoo, kuwachanja ili wasipate tetenasi  (tetanus),tunawatibu macho na ngozi ambapo kwa sasa wanaendelea vizuri," ameeleza Masija.

WITO WA ASPA KWA JAMII

Masija amewataka wanaotumia Punda katika kuwasaidia shughuli zao wawe na huruma kwa kuhakikisha wanawapatia mahitaji muhimu yanayostahili.

"Watu ambao wanawatumia Punda kuwapelekea mizigo yao sokoni wasiwabebeshe mizigo mikubwa bali kulingana na uzito wao, usizidi uzito wao na kusababisha kushindwa kutembea," amebainisha.

Amefafanua kuwa Punda anapobebeshwa mzigo mkubwa anashindwa kutembea na kudondoka na wengine wanakufa na hawezi kuongea kama mzigo huo ni mkubwa ataendelea kupigwa.

Masija amefafanua kuwa Punda wengi wamekuwa wakifa kwa kuugua magonjwa mbalimbali yakiwamo ya tetenasi.


Mbarwa Kivuyo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Inades-Formation Tanzania (IF TZ), ameeleza kuwa katika shughuli zao ambazo wanazifanya wamekuwa wakiangalia upande wa sera ni kwa namna gani wanaweza kushawishi sera hiyo ambayo itakuwa ni sheria kwa watumiaji wa Punda na wa wamiliki.

"Kuwe na sera ambazo  zitawafanya wanaotumia na wanaomiliki Punda ili waweze kutambua zile haki tano za mnyama punda, pamoja na kutumia, kuwapo na sera ambayo itakulazimisha kuziheshimu sera hizo na haki zao," amesema.

Ameongeza kuwa kutokusaminiwa kwa punda ni kwa sababu ya mtazamo wa watu kuona kwamba mnyama huyo hana thamani katika jamii.

Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa wakitoa elimu kwa jamii  juu ya umuhimu wa mnyama punda wataelewa anawapatia  kipato fulani hivyo watabadilisha mitazamo yao.

Akizungumzia upatikanaji wa dawa Kivuyo, amesema kuwa hapa nchini hawaja tambua umuhimu wa  dawa za kutibu mnyama punda dawa hizo hazipatikani katika maduka ya dawa za mifugo huku akitolea mfano nchi jirani ya Kenya zinapatikana.

Mtafiti Mwandamizi wa Mifugo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Gilbert Msuta amesema mchango wa mnyama Punda kwenye huduma za kijamii kwa jamii zinazomtegemea mnyama huyo ni mkubwa.

Amefafanua kuwa kupotea kwa mnyama huyo kutasababisha umasikini mkubwa kwenye jamii ambazo zinamtegemea Punda.

KUBORESHA USTAWI WA PUNDA

Akizungumzia uboreshwaji wa Ustawi wa mnyama Punda amesema wanaona kuna kila sababu ya kutafuta mikakati ya kudumu ya kutoa elimu kwa wafugaji na wakodishaji wa Punda.

"Watu hawa wanahitaji juhudi za makusadi kufikiwa kupewa elimu juu ya matunzo na Ustawi wa mnyama Punda," ameeleza Mtafiti huyo.

Mtafiti huyo Mwandamizi ameongeza kuwa suala la matunzo kwa mnyama Punda linahitaji kuzingatiwa kutokana na kushambuliwa na magonjwa mbalimbali.

Akizungumzia wataalamu wa mnyama Punda amesema wengi hawana utaalamu wanatibu kwa kutumia uzoefu walionao wa wanyama wengine.

"Watoa huduma wengi tuliowauliza  walisema  wakati ule mitaala ya kimatibabu hayakuzingatia matibabu ya mnyama Punda," amesema Msuta.

TAKWIMU

Msuta amesema suala la takwimu waliliona na kwamba zilizopo hazikuwa zina akisi uhalisia ambapo waliona ni muhimu kuja na mkakati wa kuanzisha utaratibu wa kuwa na takwimu sahihi za matibabu, upasuaji, za biashara ili ziweze kutoa taarifa kwa watunga sera kufanya maamuzi ambayo ni sahihi.

Ameongeza kuwa Punda akishika mimba anaitunza kwa kipindi miezi 12 hadi 14 ndio anazaa na analea mtoto miaka miwili hivyo inasababisha ongezeko lao kuwa dogo na akiwa analea hataki kupandwa na dume.

Sifa za mnyama Punda atazaa pale anapoona mazingira aliyopo yapo salama na akiona kitu chochote hakipo sawa hawezi kushika mimba.

Punda akiwa na mawazo kidogo hawezi kushika mimba hivyo sababu hizo zinachangia kwa kiasi kikubwa kuzaliana kwa kasi ndogo.

"Tunahitaji kufanya sensa ya mnyama Punda ili tuwe na maamuzi sahihi, kwa pamoja kama wadau tusimamie ustawi wa mnyama Punda," amesema.


Naye Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania (VCT), Dk. Amani Kilemile amesema kuwa watoa huduma wengi wanaangalia biashara hawawezi kuingiza dawa ambayo itakaa muda mrefu miezi mitatu au sita wanaepuka kuagiza hizo.

 "Nafikiri kuna haja ya kuangalia hasa  nyie ASPA na IF TZ ambao mnahusika  moja kwa moja kwa kutoa huduma ya hawa wanyama ambao wamesahaulika kwenda kupewa idhini ya kuingiza haya madawa, kuwategemea wafanyabiashara ni mara chache kuyapata," amesema Dk.Kilemile.

Aidha ameziomba taasisi hizo kuongea na Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo (DVS),kama wanaweza kupewa vibali ili waagize wao kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).

Akizungumzia kanuni za mifugo, Mchumi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Juma Nyabenda ameeleza kuwa kanuni inakataza kuchija majike wachanga.

"Ukitazama ongezeko la majike linalopatikana vinavyopatika kwenye uchinjaji utajua tu, tunajaribu kufuatilia tukiweza kupata ripoti nzuri ya kitafiti itatusaidia sisi watunga sera kwa namna gani tutaenda kutekeleza kanuni yetu  inayozungumzia kuhusu uchinjaji wa wanyama wenye mimba na majike," Amesema.

Mtafiti wa Mifugo na Mkurugenzi wa utafiti  kutoka TALIRI, Andrew Chota amesema kuwa wanaona umuhimu wa kuwa na sensa maalumu ya mifugo ili waweze kupata namba ya mifugo kwa  kila  nambari kwa lengo la kujua ipo mingapi na kuweka utaratibu wa namna gani inavyoweza kuhudumiwa.

"Wanyama kama Punda namba yake haifahamiki vizuri wapo wangapi nchini na wanahitaji kupewa huduma zipi," ameeleza Chota.

Ameongeza kuwa wana hitaji kufanya utafiti huo na kwamba watahitaji kufanya sensa hiyo ili kuweke mipango mizuri ya kuwahudumia wanyama hao.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU