Na Mwandishi Wetu,Chemba
SERIKALI inaendelea na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, wananchi wilayani Chemba wameelimishwa juu ya athari za kumalizana kinyumbani kesi za ubakaji, ulawiti na mimba za utotoni.
Afisa mradi msaidizi kutoka asasi ya Counsenuth, Karim Kapama amesema kuwa licha ya jitihada wanazofanya kuelimisha umma juu ya ukatili wa kijinsia, baadhi ya kesi zimekuwa zikimalizwa katika ngazi ya familia na hakuna hatua inayochukuliwa dhidi ya watuhumiwa wa maovu hayo.
"Tumekuwa tukizunguka kwenye vijiji mbalimbali wilayani Chemba kuelimisha wananchi juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia. Changamoto kubwa inayojitokeza ni kwamba wahanga wa matukio hayo wamekuwa hawapati haki wanayostahili kwani wazazi na walezi wamekuwa wakimalizana kinyumbani badala ya kufikia mahakamani." Amesema Karimu.
Afisa mtendaji Wilaya ya Chemba Siwema Juma ameishukuru asasi ya Counsenuth kwa uelimishaji umma juu ya matukio ya ukatili wa kijinsia na amewasihi kuendelea na kampeni hiyo ya kutokomeza ukatili wa kijinsia wilayani humo.
"Kumekuwa na mabadiliko makubwa tangu Counsenuth waanze kuelimisha jamii. Tunaona wanaume wameanza kuelewa madhara yanayotokana na ukatili wa kijinsia. Na Imani huu utakuwa mwanzo wa usawa wa kijinsia"
Afisa mtendaji wa kata ya Paranga Asha Hamisi amekemea vikali tabia ya kumalizana kinyumbani kwa makosa ya ukatili wa kijinsia yanayofanyika. Amesema hayo kwenye mkutano wa kuelimisha wananchi juu ya kupiga vita ukatili wa kijinsia.
"Unakuta mtoto anafanyiwa ulawiti au ubakaji lakini wazazi wanakaa kumalizana kinyumbani kwa kulipa fedha na mifugo kunyamazish ukatili huo. Watu wanaendelea na matendo maovu kwa sababu uwezo wa kuukwepa mkono wa sheria," ameeleza.
Metilda Nicholas ambaye ni Afisa polisi dawati la jinsia wilaya ya Chemba ameeleza kuwa kesi za ukatili wa kijinsia zimekuwa zikiishia njiani inapofika wakati wa kutoa ushahidi mahakamani, wahanga wa ukatili wa kijinsia wamekuwa wakiishia njiani.
"Tumekuwa tukitafuta taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia katika kaya mbalimbali. Kesi zinazobainika zimekuwa zikiishia njiani kwa kukosa ushahidi. Elimu kwa umma inahitajika ili kuwapa wananchi nafasi ya kujifunza njia sahihi ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia" amesema.
Matukio hayo ya ulawiti, ubakaji na mimba za utotoni umehusishwa na ugumu wa maisha. Wananchi wamekuwa wakipokea, fedha na mifugo ili kunyamazia ukatili wa kijinsia.
0 Comments