CHANJO YA POLIO KUANZA SEPTEMBA 21, WATOTO 3,250,598 KUCHANJWA

Na Asha Mwakyonde, Dodoma

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imetoa rai kwa wazazi na walezi kutoa ushirikiano kwa watoa huduma za afya ili kuwezesha watoto wao kuchanjwa  chanjo ya ugonjwa wa Polio kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba.

Watoto 3,250,598 waliozaliwa baada ya mwaka 2016 wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya ugonjwa wa Polio ili  kuwakinga dhidi ya Kirusi cha Polio aina ya pili (Polio Virus Type 2) kinachoweza kusababisha ulemavu wa kudumu. 

Akizungumza jijini Dodoma leo Septemba 8,2023 kuhusu kampeni ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio Waziri wa Afya Ummy  Mwalimu amesema kuwa 
Kampeni hiyo itafanyika kwa muda wa  siku nne kuanzia Septemba 21 hadi  24 , 2023 katika Mikoa sita inayopakana na nchi zenye mlipuko wa Polio ambayo ni Rukwa, Kagera,Kigoma, Katavi, Songwe na Mbeya.

Amefafanua kuwa  Mei 26,2023, Wizara ilipokea taarifa za uwepo wa mtoto mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi kumi na moja ambaye alionyesha dalili za kupooza kwa ghafla. 

"Mtoto huyu alitolewa taarifa kutoka Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.Uchunguzi wa Maabara ulithibitisha kuwa mtoto huyu ana maambukizi ya virusi cha Polio," amesema.

Waziri Ummy ameeleza Wizara inawahimiza wananchi kuendelea kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Polio kama inavyoshauriwa na wataalam wa afya kwa kuwahi katika kituo cha kutolea huduma za afya mapema kwa ajili ya uchunguzi na matibabu mara tu unapoona dalili za kupooza kwa ghafla.

Amesema kuwa tahadhari nyingine wanazotakiwa kuchukua wananchi hao ni  kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono ili kujikinga na magonjwa mbalimbali ya kuambukiza, Kuhakikisha matumizi sahihi ya vyoo bora wakati wote, na Kuhakikisha watoto wote wanapata chanjo kulingana na ratiba ili kuwakinga dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.


"Natumia fursa hii kutoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya za Tanzania Bara zitakazohusika na zoezi hili kusimamia kwa karibu maandalizi na utekelezaji wa kampeni hii kupitia Kamati za Afya ya Msingi ngazi za Mikoa 
na Wilaya. Nakuongeza kuwa,

Nawaelekeza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuhakikisha upatikanaji wa chanjo, vifaa na mafunzo kwa wataalam watakaohusika katika utoaji wa chanjo," amesema Waziri Ummy.

Aidha Waziri huyo amesema wakati wa Kampeni hiyo kutakuwa na timu yenye jumla ya watoa huduma za afya 5,291 kwa Mikoa yote sita itakayofikiwa na zoezi hilo ambapo kila timu itakuwa na watoa huduma watatu. 

Waziri Ummy ameongeza kuwa ili kufanikisha kampeni hiyo Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), pamoja na Wadau wa chanjo imeshafanya maandalizi kwa ajili ya kuwezesha zoezi hilo kuendeshwa bila kuathiri shughuli zingine za wananchi. 


Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Profesa  Tumaini Nagu amesema  timu ya watoa huduma 5,291  ya chanjo  tayari imeshapata mafunzo kutoka katika Mikoa hiyo sita.

Ameongeza kuwa lengo ni kuhakikisha watoto wote wanafikiwa kwa kupatiwa Chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio ili kuepuka kupata madhara ya ulemavu.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU