NA ANDREW CHALE, ZANZIBAR.
BAADHI ya Wananchi wa Fujoni katika Shehia tatu ikiwemo hiyo ha Fujoni, zingwezingwe na kiomba mvua wamefunguka mambo mbalimbali kwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe Ayoub Mohammed Mahmoud wakati wakiwasilisha kero mbalimbali zinazowakabiri.
Awali akitoa kero zake mbele ya Mkuu wa Mkoa, Bi. Fatma Haji Machano kutoa Shehia ya Zingwezingwe, amelalamikia kukosa huduma muhimu nyati za usiku kutokana na kituo cha Afya kukosa nyumba ya Daktari.
"Kumekuwa na kero kubwa, kua wakati Wazazi wanajifungulia njiani. Tujengewe nyumba ya Daktari" amesema Bi. Fatma.
Nae Sudi Hamza wa Shehia ya Kiomba mvua ameweza kulalamikia kero ya miundombinu ya maji, uhalifu wa wizi wa mazao na mifugo Hali ambayo inatishia usalama wao.
Ambapo pia amelalamikia suala la Bar ya vileo ya Mabatini ambayo imekuwa chanjo cha mmong'onyoko wa Maadili.
Kwa upande wake Bi. Mariam Mjaka amelalamikia moja ya Bar ya vileo ya mwanamama Bi.Mariam ambayo imekuwa ikichangia vitendo viovu ambapo wameomba kuondolewa ilikulinda maadili.
Nae Aziza Mkubwa wa Shehia ya Kiomba mvua, ambaye ni Voluntia wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (Red Cross) amelalamikia ubaguzi wa ajira za muda kwa wao vijana wa huduma ya kwanza katika miradi hiyo a baadala yake wamepewa vijana wengine kutoka mjini.
Kwa upande wake,Mbwana Said wa Shehia ya Fujoni, amelalamikia tathimini katika mradi wa maji, ambapo bado hawajalipwa.
"Miradi imepita kwa mashamba yetu, ila hatujalipwa.
Lakini pia kumejuwa na kero ya kuambiwa kuwa majina yamekosewa katika vyeti vya kuzaliwa watoto huku wakitaka pesa tsh 20,000 ili kufanya marekebisho, tunaomba suala hili kuangaliwa Mhe Mkuu wa Mkoa. " amesema Mwananchi huyo.
Nae, Ali Haji Abdalla wa Fujoni amelalamikia ndege aina ya kunguru kuharibu mazao ambapo wameomba namna ya kuona Serikali itadhibiti.
Ali Rashid Ali wa Fujoni amelalamikia hatua ya usafiri wa umma ambao wamekuwa wakiwashusha nje ya mji hali ambayo wanyonge inawakwa kwa kutakiwa kulipia usafiri zaidi ya mara mbili,
Hata hivyo, RC Ayoub ameweza kupokea maoni na kero hizo za wananchi hao na kutolea ufafanuzi huku kero zingine akisimamisha watendaji aliofuatana nao.
Aidha, akijibu kero suala la uhamiaji, Bi.Tatu Burhan Mrakibu uhamiaji mkoa wa Kaskazini Unguja anashauri kutowa taarifa kwa mgeni yeyote anaeingia katika maeneo hayo, kwani licha ya kuwa wamezungukwa na bahari amewaomba wananchi wakiona wageni ambao wanawatilia shaka kutoa taarifa kwa viongozi wa maeneo yao.
Kwa upande wake, Afisa kilimo Juma Kona Mosi amesema kwa sasa kama Serikali inaendelea kuchukua hatua katika kilimo ikiwemo kulinda mimea ya zao la mkarafuu ambayo imekuwa ikikumbwa na tatizo la kukauka huku suala la kunguru akiomba wananchi kuendelea kutumia njia mbadala kudhibiti tatizo hilo kwani kwa sasa bado Serikali haijakuja na mradi mwingine wa udhibiti kunguru hao kama ilivyokuwa hapo awali.
0 Comments