WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), umeboresha utoaji wa huduma zake kwa kuhamishia mtandaoni huduma ya usajili wa haki ya dhamana inayowekwa juu ya mali za kampuni (Charges), hatua inayolenga kuongeza ufanisi, kuharakisha huduma na kupunguza ulazima wa wateja kufika ofisini.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na BRELA leo Julai 23, 2026, huduma hiyo sasa inapatikana kupitia mfumo ulioboreshwa wa BRELA Online Service (BOS), ambapo kampuni, taasisi za kifedha, ofisi za wanasheria pamoja na wadau wengine wanaweza kuwasilisha maombi yao kwa njia ya mtandao.
BRELA imeeleza kuwa awali huduma hiyo ilihitaji mteja kufika katika ofisi za wakala ambapo maboresho yaliyofanyika sasa yanawawezesha wateja kuwasilisha nyaraka zote zinazohusu usajili wa haki ya dhamana bila kufika ofisini.
Kwa mujibu wa utaratibu mpya, mwombaji anatakiwa kwanza kufungua akaunti kwenye mfumo wa BOS, kisha kuchagua huduma za kampuni (Company Services),na kuingia kwenye kipengele cha huduma za dhamana (Charges Services), ambapo atachagua huduma ya Registration of Charges.
Imesema kuwa baada ya hapo, mteja atabofya sehemu ya Register New Charges, ataingiza namba ya usajili wa kampuni husika na kuendelea kujaza taarifa zinazohitajika, ikiwemo Fomu Na. 99 inayopatikana kupitia tovuti ya BRELA.
Aidha, BRELA imewataka wateja ambao bado hawajafungua akaunti katika mfumo wa BOS kufanya hivyo kwa kutembelea mfumo huo na kubonyeza sehemu ya Create New Account.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa baada ya kujaza taarifa zinazohitajika, mtumiaji atapokea ujumbe mfupi pamoja na maelekezo kupitia barua pepe yatakayomwezesha kuanza kutumia mfumo huo wa kidijitali.
Wakala huo umebainisha kuwa maboresho hayo ni sehemu ya jitihada za kuendelea kurahisisha mazingira ya kufanya biashara nchini kwa kutumia teknolojia ya kidijitali, sambamba na kuhakikisha huduma zinapatikana kwa haraka, kwa urahisi na kwa ufanisi zaidi.
BRELA imewahimiza wateja wanaohitaji msaada kuwasiliana kupitia namba ya simu +255 (0)22 2212800 au kutuma barua pepe kwa support.bos@brela.go.tz.

0 Comments