Na Asha Mwakyonde
MAADHIMISHO ya Wiki ya Huduma za Fedha yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga kupata elimu ya fedha na kufahamu fursa mbalimbali za mikopo zinazolenga kuchochea maendeleo ya kiuchumi, huku wakihimizwa kujitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho hayo yanayoendelea katika viwanja vya Usagara.
Wiki ya huduma za fedha yawafungulia wananchi wa Tanga milango ya elimu na mikopo.
Meneja Masoko na Uhamasishaji kutoka Mfuko wa SELF Microfinance Fund (SELF MF),
Linda Mshana amesema ushiriki wako katika wiki ya huduma za fedha unalenga kuwajengea uwezo wananchi mbalimbali waliomtolea banda la mfuko huo.
Hayo ameyasema Januari 20,2026 wakati akizungumza na wananchi waliotembelea banda la mfuko huo katika maadhimisho hayo
huku akisema maadhimisho ya huduma za fedha yamelenga kuwajengea wananchi uelewa sahihi kuhusu masuala ya fedha, hususan matumizi bora ya mikopo.
Ameeleza kuwa ni pamoja na mambo ya msingi ya kuzingatia kabla ya kukopa pamoja na maswali muhimu wanayopaswa kuyauliza wanapohusiana na taasisi za kifedha kwa lengo la kuepuka mikopo yenye riba kubwa na masharti yasiyokuwa rafiki kwao.
Ameeleza kuwa Mfuko wa SELF unaendelea kutoa mikopo ya aina mbalimbali inayolenga kuwawezesha wananchi kiuchumi, ikiwemo mikopo kwa wafanyabiashara wa sekta ya nafaka, wakulima, wafugaji na wavuvi.
"Mfuko huu unatoa mikopo ya kuboresha makazi kwa wananchi wanaohitaji kuboresha au kukarabati nyumba zao," anaeleza Mshana.
Amefanunua kuwa wanatoa mikopo kwa taasisi za kifedha ambazo tayari zimeanzishwa na zina vibali halali vya Benki Kuu ya Tanzania (BoT),kwa lengo la kuongeza mtaji na kuziwezesha kutoa huduma kwa wananchi wengi zaidi.
Ameongeza kuwa maswali kuhusu riba yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara miongoni mwa wananchi, hali inayoonesha bado kuna uhitaji mkubwa wa elimu ya fedha, hasa katika kukokotoa riba na kuelewa masharti ya mikopo kabla ya kuingia kwenye mikataba ya kifedha.
Mshana amesisitiza kuwa Mfuko wa SELF utaendelea kutoa elimu na mafunzo ya masuala ya fedha na bima kama sehemu ya jitihada za Serikali za kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi na kufikia maendeleo endelevu.
Amefafanua kuwa Mfuko wa SELF ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Fedha, inayolenga kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu sambamba na elimu ya fedha kwa maendeleo endelevu ya jamii.

0 Comments