WANAWAKE ILAZO MBUYUNI WANAVYOUPINGA MISEMO ISIYO NA TIJA

Na Asha Mwakyonde,Dodoma

UPO usemi usemao 'Wanawake hawapendani' usemi huu  hapo awali ulikuwa ukileta taswira mbaya katika jamii na kufifisha juhudi za kimaendeleo zinazofanywa na baadhi ya wanawake.

Lakini kutokana na ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia usemi huo hauna ukweli wowote kwa kuwa wanawake wengi katika dhama hizi wamekuwa wakijishughulisha na mambo mbalimbali  yakiwamo kujiunga katika vikundi vya kuwezeshana kiuchumi, kusaidiana katika shida na raha kama vile sherehe na maafa yanapotokea.

Haya yamejidhihirisha katika kikundi cha wanawake cha Peace and Love kilichopo Ilazo Mbuyuni mtaa wa sokoni Kata ya Ipagala Jijini Dodoma chenye wanachama 21 idadi ambayo haijawahi kubadilika tangu kuanzishwa kwa kikundi hivyo.

Hivyo kutokana na umoja wao wa kusaidiana kwenye shida na raha, kukopeshana kwa mtu mmoja mmoja pamoja na kuwa miradi ya kikundi wanachama hao wameweza kupata mafanikio makubwa katika familia zao.

Mary Mayemba maarufu kama Mama  Nanka ni Mwenyekiti wa kikundi hicho ambacho kilianzishwa mwaka 2015 kikiwa na lengo la kuteta umoja na ushirikiano kwa wanawake wa eneo hilo.

Amesema madhumuni ya kikundi hicho ni kusaidiana, kushirikiana na kufarijiana kipindi cha shida na raha   kama   misiba na sherehe.

Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa chanzo cha mapato yao ni   wananchama kulipa ada ya kila mwezi, kukopeshana fedha kwa riba huku akifafanua kwamba riba hiyo inawasaidia kuongeza fedha kwenye kikundi hicho.

Ameongeza kuwa vyanzo vingine vya mapato  vinatokana na miradi ya kukodisha viti, kupika kwenye shughuli mbalimbali  kama sherehe na matukio mengine.


"Pia kama kikundi tuna mradi wa kufunga kuku ambao unatuingizia fedha kwenye kikundi chetu cha peace and love," amesema Mayemba.

Ameongeza kuwa chama hicho tayari kimeshasajiliwa na kupata mkopo wa asilimia 10 unaotolewa na  Halmashauri kwa  wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mwenyekiti huyo amefafanua kuwa mkopo wa awamu ya kwanza walipata milioni 2, ambao uliwasaidia kuanzisha biashara za kikundi na awamu ya pili walipata milioni 10.
Amesema kuwa wanachama wao wapo vizuri, wanajitambua na kwamba wakichukua mikopo wanaielekeza katika malengo ya msingi waliojiwekea.

Mwenyekiti huyo amefafanua kuwa mikopo wanayoichukua wanakikundi hao wanaitumia kwa kulipa ada za watoto wao na kuendeleza biashara zao.

Akizungumzia usemi usemao 'Wanawake hawapendani' ameeleza kuwa  hauna maana yoyote kwani wao wameungana wanawake kwenye kikundi  wanapendana na wanakopeshana. 

CHANGAMOTO 

Akizungumzia changamoto za kikundi hicho mwenyekiti huyo ameeleza kuwa baadhi ya wanakikundi kuchelewa marejesho kutokulipa kwa wakati.

"Lakini hatuna changamoto kubwa mtu anaweza akachelewa mwezi huu asilete marejesho mwezi ujao akajitahidi  akaleta hivyo sidhani kama tuna changamoto kubwa," amesema.


MATARAJIO

Amesema matarajio yao ni  kuwa na  mfuko mkubwa wenye michango mingi ya fedha ili waweze kuanzisha biashara ambayo itawasaidia wanachama na jamii ya watu weye uhitaji.

"Pia matarajio yetu  mengine ni kuona kikundi chetu  kinafahamika zaidi hadi serikalini pamoja na kuisaidia jamii," ameeleza.

HALI ZA MAISHA ZA WANAKIKUNDI

Akizungumzia maisha ya wanakikundi hao mwenyekiti huyo amesema hali zao kiuchumi zimebadilika tofauti na awali kabla ya kuanzishwa kikundi hicho.

Ameongeza kuwa awali baadhi ya wanachama wa kikundi hicho hawakuwa na biashara ambapo kwa sasa wameanzisha biashara zao ambazo zinawaingizia kipato.

Hata hivyo akizungumzia usemi wa 'wanawake hawapendani' Mwenyekiti huyo amesema  kikundi hicho ni cha wanawake endapo ikitokea migogoro wanakaa na kufanya suluhisho kwa lengo kuendelea na majukumu yao.

"Kwenye vikundi kama hivi hasa vya wanawake migogoro huwa haikosekanani sisi tunakaa chini na kuongea na baadae kufikia muafaka," ameeleza.

WITO WAKE KWA WANAWAKE

Amewataka wanawake ambao hawapo kwenye vikundi wahamasishane na kujiunga na vikundi kama hivyo ili waweze kufanya vitu ambavyo vitawaletea maendeleo yao binafisi, familia na Taifa kwa ujumla.

"Kama mwanamke ukikaa na kusema siwezi hutoweza na mkiungana wanawake wengi kila mtu anakuja na wazo lake mkichanganya pamoja mnapata wazo ambalo mtalifanyia kazi na kuwa na manufaa kwenye kikundi," amesema.

Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa mwanamke hapaswi kukata tamaa bali kupambana ili kuendeleza familia na kuiweka katika mazingira bora.

Siku Mwanakatwe  maarufu Mama Mwana ni muweka hazina wa kikundi hicho cha peace and love amesema wanakikundi wanajitahidi kutoa ada ya kila mwezi pamoja na fedha za maafa.

Mwanakatwe amefafanua kuwa wametenganisha mfuko wa ada na maafa huku akisema fedha za ada zinaingizwa kwenye  fedha za mkopo na kwamba za maafa zinabaki kwa ajili ya kuhudumia wanakikundi watakaopata maafa mbalimbali.

Akizungumzia urejeshaji mikopo kwa wanakikundi hao ameeleza kuwa wanarejesha mikopo yao kama walivyokubaliana na kwamba kwa wale wanaosuasua wanawakumbusha kulipa marejesho yao.

"Riba ambayo inapatikana kutoka kwenye mikopo  mwishoni mwa mwaka wanakikundi wanarejeshewa na kupitia riba hii  wanatoa asilimia fulani kulingana na riba ya mwanakikundi ambayo inatumika kujazia mfuko," amesema.

Ameongeza kuwa riba ambayo inapatikana kutokana na fedha za maafa inakuwa ni mali ya chama huku akifafanua kwamba inasaidia mwanakikundi kukopa pale anapopata dharura ya kurejesha mkopo mkuu.

"Fedha zinazotokana na mfuko wa maafa wakati mwingine zinatumika kama kufanya sherehe mwisho wa mwaka," ameeleza Mwanakatwe.

Aidha amewataka wanakikundi ambao wanasuasua katika urejeshaji wao kwa kuwa fedha hizo zinawasaidia wanakikundi wote.

Kwa upande wake mwanakikundi hicho  Winifrida Omary ameeleza kuwa mkopo anaouchukua katika kikundi unamsaidia kuwalipia  watoto wake  ada pamoja na mahitaji mengine.

" Kisingekuwepo kikundi hiki sijui ningekuwa wapi mimi ni mjane nimeachiwa watoto kimenisaidia nimefungua mgahawa wangu kupitia fedha za mkopo wa kikundi hiki," amesema.

Akizungumzia matarajio yake amesema ni kuwa na  vyombo kwa ajili ya kutoa huduma ya vyakula kwenye sherehe mbalimbali huku akisema anaimani atapata fedha kupitia kikundi hicho ili kutimiza malengo yake.

Naye Ester Enock  ambaye ni mwanakikundi na Mwenyekiti Msaidizi ameeleza kikundi hicho kinawasaidia kuwezeshana mikopo ambayo wameitumia kuanzisha na kuendeleza  biashara zao binafisi.

Amefafanua kuwa kabla ya kuazishwa kikundi hicho tayari   alikuwa na biashara ambapo baadae aliongeze mtaji wake baada ya kukopeshwa fedha.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI