TAASISI ZA UDHIBITI ZAELEKEZWA KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI YA UFANYAJI BIASHARA NCHINI

                       Morogoro 

TAASISIS za Udhibiti zimeelekezwa kuweka mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara nchini ikiwa ni jukumu kuu na la msingi ili kutatua kero za wafanyabiashara na wawekezaji kwenye sekta mbalimbali badala ya kuwa kikwazo na endapo kuna sheria, kanuni na taratibu zenye mikinzano zirekebishwe.          

Wito huo umetolewa na Dkt. Hashil Abdallah, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, alipokuwa akifunga kikao kazi kilichohudhuriwa na Taasisi za Udhibiti leo tarehe 15 Septemba, 2023 jijini Morogoro ambapo kikao hicho kiliratibiwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).        

Dkt. Abdallah amesema kuwa Taasisi za Serikali zinatakiwa kuzungumza kimifumo hasa katika maeneo yanayohusiana kiutendaji ili kumsaidia ambaye anataka kufanya baishara au kuwekeza nchini na kupata huduma kwa kasi kwakuwa uchumi wa nchi unakuwa kwa kutegemea mazingira bora ya ufanyaji biashara nchini na kuchochewa kuanzia ngazi ya Taasisi.        

“Tuhakikishe uwezeshaji wetu unaendana na kasi za utatuzi wa kero zinazozungumziwa ni jukumu letu kuzitatua na Wizara yetu ambayo imepewa dhamana ya kusimamia sekta hii pamoja na Taasisi zilizo chini yake, itaendelea kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazoathiri uanzishwaji na ufanyaji wa biashara”, ameeleza Dkt. Abdallah.

Ameendelea kusema kuwa Wizara kupitia Taasisi zake itaendelea kukutana mara kwa mara na wadau wa biashara  ili kupokea changamoto zao pamoja na kuwapatia mrejesho wa hatua mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali kuboresha sekta ya biashara.      

Dkt. Abdallah amesisitiza kuwa ili kufanikisha  utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Sita Wizara ya Viwanda na Biashara inatekeleza maono hayo kwa vitendo kwa kufanya mapitio ya Sera zake hususan Sera Taifa ya Biashara ya mwaka 2003 ambayo kwa sasa iko katika ngazi ya Baraza la Mawaziri ambapo mapitio ya Sera hiyo yamezingatia wakati wa sasa wa ufanyaji biashara, mabadiliko ya sayansi na teknolojia pamoja na malengo ya Jumuiya mbalimbali za Kikanda na Kimataifa ambazo Tanzania imeridhia kuwa mwanachama.      

Ameongeza kwa kusema kuwa mageuzi hayo yanayofanywa na Serikali, yanalenga pia kuwawezesha wazalishaji wa bidhaa na wafanyabiashara  kuzifikia fursa mbalimbali za masoko ya Kikanda na Kimataifa ili kukuza mauzo ya nje na kuiwezesha nchi  kuongeza wigo wa ajira na fedha za kigeni.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa,   amemuhakikishia kuwa BRELA itawasilisha rasmi Wizarani maazimio yote ya kikao ili hatua mbalimbali zichukuliwe katika maeneo ambayo yanahitaji uboreshaji na kufikiwa maamuzi kwa haraka. 

BRELA imekutana na Taasisi za Udhibiti ili kujadili mikakati ya pamoja ya namna ya kutatua mikinzano inayojitokeza katika utendaji kazi wa kila siku, kutokana na Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia Taasisi hizo hapa nchini, Kikao kazi hicho kilianza tarehe 13 Septemba, 2023 hadi 15 Septemba, 2023.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU