Na Asha Mwakyonde, DODOMA
MBUNGE wa Viti Maalum, Nasriya Nasir Ali, ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa juhudi zake za kuboresha sekta ya elimu, hususan kwa kuandaa miongozo tisa inayolenga ujumuishaji wa watu wenye ulemavu katika mfumo wa elimu nchini.
Hayo ameyasema leo Mei 8,2026 wakati akichangia hoja katika bajeti ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Nasriya amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa itarahisisha utoaji wa elimu kwa watoto wenye ulemavu na kuwapa fursa sawa ya kupata elimu bora, akisisitiza kuwa elimu ndiyo ufunguo wa maisha kwa kila mwananchi bila kujali hali yake.
Aidha, amempongeza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda pamoja na Naibu Waziri, Wanu Hafidh Ameir, kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuimarisha elimu jumuishi nchini.
Amesema ana imani viongozi hao wataendelea kusimamia vyema utekelezaji wa miongozo hiyo ili kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanajumuishwa kikamilifu katika shule za kawaida na maalum.
Nasriya ameiitaka Serikali kujenga shule jumuishi katika kila mkoa na wilaya ili kupunguza changamoto kwa wazazi wanaolazimika kuwapeleka watoto wao kusoma mbali na maeneo wanayoishi.
Amesema umbali mkubwa wa shule hizo unasababisha gharama kubwa pamoja na kupoteza muda kwa wanafunzi wenye ulemavu.
“Nilikuwa naishi Zanzibar lakini nilisoma Tanzania Bara. Wakati huo shule ya msingi kwa baadhi ya watoto wenye ulemavu ilikuwa ni miaka 10 kabla ya kuendelea sekondari. Hii ilikuwa changamoto kubwa kutokana na umbali na mazingira ya masomo. Niombe shule hizi zijengwe kila mkoa na wilaya ili kupunguza gharama na changamoto kwa watoto hawa,” amesema.
Akizungumzia lugha ya alama, Nasriya ameomba somo hilo lifundishwe rasmi kuanzia elimu ya awali hadi vyuo vikuu ili kuwasaidia watoto wenye ulemavu wa kusikia kupata elimu kwa urahisi zaidi.
Amesema pamoja na uwepo wa walimu na wakufunzi, bado kuna haja kubwa ya kuwawezesha kwa mafunzo maalum ili waweze kuwafundisha watoto wenye ulemavu kwa ufanisi.
“Tunatamani kuona ujumuishaji wa kweli. Walimu wapo na wanafunzi wapo, lakini kuna umuhimu mkubwa wa kuwawezesha walimu hao ili waweze kuwafundisha watoto hawa kwa njia sahihi,” amesema.
Hata hivyo, ameiomba Ofisi ya Mkurugenzi ndani ya Wizara ya Elimu kuendelea kushirikiana kwa karibu na vyama vya watu wenye ulemavu ili kupata mawazo na ushauri utakaosaidia kuboresha mfumo wa elimu nchini.
Aidha ameipongeza wizara hiyo kwa kuanzisha mitaala mipya ya elimu, akieleza kuwa kuna aina mbalimbali za ulemavu zinazohitaji mifumo tofauti ya ufundishaji.
Amefafanua kuwa watoto viziwi hukaa muda mrefu zaidi katika elimu ya msingi kutokana na mahitaji yao maalum, hali inayowafanya wakati mwingine kushindwa kumaliza masomo kwa wakati.
Nasriya amesisitiza kuwa maboresho ya mitaala yanapaswa kuzingatia pia namna ya kufanya tathmini na usahihishaji wa mitihani kwa watoto wenye ulemavu, hususan wenye changamoto za lugha.
Ameeleza kuwa ni muhimu kwa wizara kushirikisha wadau wa elimu na vyama vya watu wenye ulemavu wakati wa kuandaa miongozo na programu mbalimbali za elimu kwa kuwa wao ndio wanaofahamu changamoto wanazokutana nazo.
“Nimetembelea mikoa mbalimbali na kuona shule za watu wenye ulemavu. Kuna maeneo miundombinu bado si rafiki kwa watoto hawa. Ni muhimu iboreshwe ili waweze kusoma katika mazingira bora,” alisema.
Akizungumzia mpango wa bima ya afya kwa wote, Nasriya alisema ni vyema watoto wenye ulemavu waliopo mashuleni, hasa shule za bweni, wakapatiwa bima za afya kutokana na mahitaji yao maalum.
Ameiomba Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kuhakikisha suala hilo linapatiwa kipaumbele.
Aidha, ametoa mfano wa Shule ya Msingi Katumba iliyopo Tukuyu mkoani Mbeya, akisema shule hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu wa kuwafundisha watoto wenye ulemavu.
“Mimi nipo tayari kutumika kusaidia kuboresha elimu nchini kwa sababu ninaelewa changamoto hizi. Wakati mwingine nakosa usingizi nikijiuliza hatma ya watoto wenye ulemavu huko mbele,” amesema.
Nasriya pia amesisitiza umuhimu wa kuwa na takwimu sahihi za watoto wenye ulemavu nchini ili kurahisisha upangaji wa huduma na ugawaji wa vifaa saidizi.
Amesema Serikali inapaswa kuhakikisha vifaa hivyo vinawafikia watoto wote wenye uhitaji katika maeneo mbalimbali nchini kwa usawa.
Ameitaka Wizara ya Elimu ya Tanzania Bara na ile ya Zanzibar kushirikiana kwa karibu ili kuboresha elimu ya watoto wenye ulemavu, akisema bado kundi hilo linakabiliwa na changamoto nyingi, hasa Zanzibar.




0 Comments