SERIKALI KUIMARISHA MAADILI YA VIONGOZI KUPITIA TEHAMA NA ELIMU


Na Asha Mwakyonde,DODOMA 

SERIKALI imeendelea kuimarisha uwajibikaji na uadilifu miongoni mwa viongozi wa umma kwa kuboresha matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) pamoja na kuongeza juhudi za utoaji wa elimu ya maadili kwa viongozi na wananchi. Hatua hiyo inalenga kurahisisha utoaji wa huduma, kuongeza uwazi na kujenga misingi imara ya utawala bora nchini, hususan katika ngazi za halmashauri.

Hayo ameyasemwa leo Aprili 17,2026 bungeni jijini hapa na waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora bora, Ridhiwani Kikwete wakati akiwasilisha kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2026/2027, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imejipanga kutekeleza vipaumbele viwili vikuu ambavyo ni kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma kwa taasisi na wananchi, pamoja na kuendelea kutoa elimu ya maadili kwa viongozi wa umma ili kukuza uwajibikaji wa pamoja.

Amesema Sekretarieti imepanga kupokea na kuhakiki matamko ya rasilimali na madeni ya viongozi wa umma kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma (Sura 398), kuchunguza tuhuma za ukiukwaji wa maadili, pamoja na kupokea na kufanyia kazi malalamiko kutoka kwa wananchi.

Aidha Waziri huyo ameeleza kuwa Ofisi hiyo itaendelea kuratibu majukumu ya Baraza la Maadili na kuhamasisha utekelezaji wa Hati ya Ahadi ya Uadilifu.

"Juhudi zitaelekezwa katika kutoa elimu kwa Umma kuhusu maadili ya uongozi, kuanzisha na kuimarisha klabu za maadili katika shule na vyuo, pamoja na kukamilisha na kuendeleza ujenzi wa ofisi za kanda mbalimbali nchini ikiwemo Mwanza, Mbeya, Morogoro na kuanza ujenzi wa ofisi ya Kanda ya Kaskazini Arusha," amesema Kikwete.

Akizungumzia mwaka wa fedha 2025/26, amesema Sekretarieti ilipokea na kutumia asilimia 63.79 ya bajeti yake kufikia Machi 2026, ambapo fedha hizo zilitumika katika shughuli mbalimbali za kusimamia maadili ya viongozi wa umma.

Ameongeza katika utekelezaji wake, jumla ya matamko ya rasilimali na madeni 15,034 yalipokelewa kwa njia ya mtandao, sawa na asilimia 85 ya matamko yaliyotarajiwa. Vilevile, malalamiko 120 kuhusu ukiukwaji wa maadili yalipokelewa na kuchambuliwa, huku baadhi yakiendelea kufanyiwa uchunguzi.

Aidha,amefafanua kuwa viongozi wa umma 258 walifanyiwa uhakiki wa matamko yao, ambapo asilimia 16.3 walibainika kuwa na kasoro na hatua stahiki kuchukuliwa. Sekretarieti pia ilitoa elimu ya maadili kwa zaidi ya wadau 26,000 kupitia mikutano na vyombo vya habari.

"Katika kuendeleza maadili kuanzia ngazi za chini, klabu mpya 170 za maadili zilianzishwa katika shule za msingi na sekondari, huku zaidi ya klabu 500 zikiimarishwa kupitia ziara na mafunzo maalum," amesema.

Ameeleza kuwa katika hatua nyingine iliyotekelezwa ni pamoja na viongozi 4,659 kusaini Hati ya Ahadi ya Uadilifu, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uwajibikaji wao katika utumishi wa umma.

Waziri huyo ameeleza kuwa kwa upande wa miundombinu, ujenzi wa jengo la Makao Makuu Dodoma umekamilika na kuanza kutumika, huku miradi ya ujenzi katika kanda mbalimbali ikiendelea katika hatua tofauti.

Kwa ujumla, hatua hizi zinaakisi dhamira ya Serikali ya kuimarisha maadili ya uongozi na kuhakikisha viongozi wa umma wanawajibika ipasavyo kwa manufaa ya taifa.

Post a Comment

0 Comments

e-GA YAJIPANGA KUONGEZA UFANISI WA HUDUMA ZA SERIKALI MTANDAO NCHINI