Na Asha Mwakyonde, DODOMA
SERIKALI kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) imeweka mkakati kabambe wa kuimarisha usalama, ufanisi na ubora wa mifumo ya TEHAMA katika taasisi za umma, hatua inayolenga kuhakikisha huduma za kidijitali zinapatikana kwa uhakika, haraka na kwa usalama kwa wananchi na taasisi mbalimbali nchini.
Hayo ameyasema leo Aprili 17,2026 bungeni jijini hapa na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora bora, Ridhiwani Kikwete wakati akiwasilisha kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2026/2027, amesema mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka huo wa fedha e-GA itaendeleza usimamizi na tathmini ya hali ya usalama wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA katika taasisi 571 za umma, sambamba na kushauri maeneo ya kuboresha na kufuatilia utekelezaji wake ili mifumo hiyo iweze kufanya kazi kwa ufanisi muda wote.
Ameeleza kuwa katika kuimarisha utoaji wa huduma, mamlaka hiyo imepanga kuboresha mifumo ya TEHAMA jumuishi, ya kisekta na ya kitaasisi ili iendelee kutoa huduma kwa ufanisi na usalama, huku ikifanya uchambuzi, usanifu na ujenzi wa mifumo mipya ya kisekta kwa taasisi zenye utendaji unaofanana ili kupunguza wingi wa mifumo isiyo na tija serikalini.
Aidha, ameongeza kwamba e-GA itaendelea kuunganisha mifumo ya taasisi za serikali kupitia Mfumo wa Government Enterprise Service Bus (GovESB),ili kuwezesha mawasiliano na ubadilishanaji wa taarifa kwa urahisi zaidi, hatua itakayochochea ufanisi wa huduma za serikali mtandao.
"Mamlaka hii imejipanga kufanya utafiti na ubunifu katika matumizi ya teknolojia mpya za TEHAMA kwa lengo la kuibua huduma mpya kwa umma pamoja na kuhakikisha matumizi salama ya teknolojia zinazoibuka," amesema.
Kwa upande wa miundombinu, amebainisha kuwa e-GA itaongeza wigo wa mtandao wa mawasiliano serikalini (Government Network) ili kufikia wilaya zote nchini, hali itakayowezesha taasisi nyingi zaidi kutumia mifumo ya serikali ikiwemo mfumo wa Ofisi Mtandao (e-Office).
Kwa mujibu wa waziri huyo mamlaka hiyo itaendelea kuimarisha mifumo ya kimkakati, kisekta na kitaasisi kwa kuhakikisha inazingatia sheria, kanuni, viwango na miongozo iliyopo, pamoja na kusimamia na kuendeleza miundombinu shirikishi ya TEHAMA ikiwemo vituo vya kuhifadhi taarifa na mifumo ya kujikinga na majanga.
Amesema katika kukuza rasilimali watu, e-GA itaongeza juhudi za kuwajengea uwezo watumishi wa umma katika usimamizi wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA, pamoja na kutoa mafunzo kwa watumiaji kuhusu matumizi sahihi na salama ya teknolojia hizo.
Mamlaka hiyo itaendelea kutoa ushauri wa kitaalamu na msaada wa kiufundi kwa taasisi za umma ili kuhakikisha matumizi ya TEHAMA yanazingatia viwango vilivyowekwa, kuongeza tija na kupunguza gharama za uendeshaji serikalini

0 Comments