PSPTB KUWAKUTANISHA WAKUU WA UNUNUZI NA UGAVI KUJADILI UTEKELEZAJI WA DIRA YA 2050


Na Asha Mwakyonde, DODOMA 

BODI ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) imeandaa mkutano maalum utakaowakutanisha wakuu wa vitengo, wakurugenzi pamoja na mameneja wa ununuzi na ugavi kutoka sekta za umma na binafsi, kwa lengo la kujadili utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 katika sekta hiyo muhimu.

Akizungumza jana jijini hapao katika ofisi ya Bodi hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Uanachama na Ushauri wa Kitaalamu wa PSPTB, Amos Kazinza, alisema mkutano huo ni jukwaa muhimu litakalowakutanisha wataalamu hao ili kubadilishana uzoefu na kujadili kwa kina namna bora ya kutekeleza dira hiyo kwa ufanisi.

“Naomba kutumia fursa hii kuuarifu umma kuhusu mkutano tulioandaa kwa ajili ya wakuu wa vitengo vya ununuzi na ugavi, wakurugenzi na mameneja wanaoshughulikia masuala haya nchini.

Tunawakaribisha kushiriki katika jukwaa hili muhimu la kujadiliana kuhusu utekelezaji wa Dira ya 2050,” alisema Kazinza.

Alifafanua kuwa lengo kuu la mkutano huo ni kuwajengea uwezo wataalamu hao ambao ndio wahusika wakuu wa maamuzi katika eneo la ununuzi na ugavi, ili waweze kutafsiri na kutekeleza kwa ufanisi miongozo ya dira hiyo kulingana na mahitaji ya sekta zao.

“Sisi kama bodi, kwa kushirikiana na wadau wetu, tumebaini maeneo muhimu yanayohitaji kipaumbele katika utekelezaji wa dira hii. Ndiyo maana tumeanza na viongozi hawa wa juu katika ununuzi na ugavi ili kujadili kwa pamoja mbinu bora za utekelezaji,” alieleza.

Kwa mujibu wa Kazinza, mkutano huo utafanyika kuanzia Juni 16 hadi 18 mwaka huu jijini Mwanza, na unatarajiwa kuwa na matukio mbalimbali ikiwemo mijadala ya kitaalamu, maonesho pamoja na majadiliano ya wazi.

Aliongeza kuwa PSPTB ndiyo taasisi inayosimamia mnyororo wa ununuzi na ugavi katika taasisi zote za umma na binafsi, hivyo ni muhimu kwa wataalamu wote walio chini ya bodi hiyo kushiriki kikamilifu katika mkutano huo.

FURSA KWA WAFANYABIASHARA 

Aidha, Kazinza alisema mkutano huo pia utatoa fursa kwa wafanyabiashara kushiriki na kuonesha bidhaa na huduma wanazotoa, kwa lengo la kupanua masoko na kujitangaza zaidi.

“Wafanyabiashara ni sehemu ya mnyororo wa ugavi, hivyo huu ni nafasi muhimu kwao kuonesha bidhaa zao na kukuza biashara zao,” alisema.

Aliwataka wadau mbalimbali kujitokeza kudhamini mkutano huo, akieleza kuwa ni mkutano wa kwanza wa aina yake unaowakutanisha viongozi wa juu wa ununuzi na ugavi nchini.

MATARAJIO YA PSPTB

Kazinza alisema wanatarajia washiriki wa mkutano huo watatoka wakiwa na uelewa mpana zaidi wa masuala ya mnyororo wa ugavi, sambamba na kuimarisha ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ndani ya taasisi wanazozihudumia.

“Lengo ni kuhakikisha wataalamu hawa wanapata uelewa wa kina wa masuala ya mnyororo wa ugavi yaliyobainishwa katika Dira ya 2050, pamoja na mbinu sahihi za kuyatekeleza,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki wasiopungua 500, akibainisha kuwa PSPTB inao wataalam wenye sifa za ukuu wa vitengo, wakurugenzi na mameneja wanaosimamia shughuli za mnyororo wa ugavi nchini zaidi ya 1,000.

Aliwahimiza wakuu wa vitengo, wakurugenzi na mameneja wa ununuzi na ugavi kuhakikisha wanashiriki ili kufanikisha malengo ya mkutano huo na kuchangia maendeleo ya sekta hiyo nchini.

Post a Comment

0 Comments

WAJUMBE WA KAMATI ZA MTAKUWWA WATAKIWA KUTOA TAARIFA SAHIHI ZA UTEKELEZAJI