SERIKALI KUANZA AWAMU YA PILI YA MSAADA WA KISHERIA, HAKI KUFIKIA KILA MTANZANIA


Na Asha Mwakyonde, DODOMA 

KATIKA hatua ya kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi wote, Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imetangaza kuanza kwa nguvu mpya Awamu ya Pili ya Kampeni ya Mama Samia ya Msaada wa Kisheria (MSLAC II), ikiwa ni mkakati mpana wa mageuzi ya mfumo wa haki nchini unaolenga kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa huduma za kisheria.

Akiwasilisha leo, Aprili 24, 2026 bungeni jijini hapa hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk.Juma Homera amesema na kusisitiza kuwa kampeni hiyo si mpango wa kawaida bali ni mabadiliko ya msingi yatakayohakikisha haki inapatikana kwa kila Mtanzania bila kujali eneo, kipato au hali ya kijamii.

Amesema kupitia MSLAC II, Serikali inajenga mfumo jumuishi unaounganisha Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, wadau wa maendeleo pamoja na jamii kwa ujumla, kwa lengo la kuhakikisha hakuna mwananchi anayebaki nyuma katika kupata haki.

Dk. Homera ameeleza kuwa utekelezaji wa mpango huo utaongozwa na misingi ya uwajibikaji, weledi na matokeo yanayopimika, huku akitoa wito kwa watendaji wa Serikali kuutambua utoaji wa haki kama wajibu wa msingi, na si huduma ya hiari.

Ameongeza kuwa Wizara imejipanga kufanya mageuzi ya kihistoria kwa kugeuza huduma ya msaada wa kisheria kuwa haki ya msingi ya kila Mtanzania, hatua itakayochochea usawa, utulivu na mshikamano wa kitaifa pamoja na kuimarisha utawala wa sheria.

Katika hatua nyingine, Dk. Homera amesema Wizara imepanga kuweka mkazo katika ujenzi wa mifumo ya TEHAMA, kuimarisha ulinzi wa mashahidi, kuongeza huduma za msaada wa kisheria, pamoja na kuendeleza rasilimali watu na kufanya mapitio ya sheria ili kuendana na mahitaji ya maendeleo na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Aidha, Dk. Homera ameeleza kuwa Serikali imeelekeza kuanzishwa kwa mfumo wa kidigitali wa kitaifa wa msaada wa kisheria (e-Legal Aid) ndani ya siku 120, ambao utawezesha usajili wa kesi kwa njia ya mtandao, ufuatiliaji wa huduma pamoja na uchambuzi wa takwimu kwa ajili ya kufanya maamuzi sahihi ya kisera na kiutendaji.

Ameongeza kuwa mfumo huo utaunganishwa na Dashibodi ya Taifa itakayowezesha ufuatiliaji wa matokeo kwa wakati halisi, kuongeza uwazi na kuimarisha uwajibikaji kwa watendaji katika ngazi zote.

Waziri huyo amesema utekelezaji wa hatua hizo utaiwezesha Tanzania kuwa na mfumo wa haki wa kisasa unaotumia teknolojia, unaojali usawa na unaohakikisha kila mwananchi anapata haki kwa haraka na kwa ufanisi, hatua inayochangia kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Post a Comment

0 Comments

VIPAUMBELE 17 KULETA MAGEUZI SEKTA YA SHERIA