Na WMJJWM, Dar-es-Salaam.
SERIKALI imeendelea na jitihada za kuimarisha Huduma za Ustawi kwa Makundi Maalum nchini kwa kuhakikisha kwamba mifumo ya kuwafikia na kuwahudumia ni rafiki.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawaka na Makundi Maalum Dkt. Seif Shekalaghe alipokua akifungua kikao kazi kilichoshirikisha wadau kutoka Wizara za Kisekta na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Oktoba 30,2023, Jijini Dar Es Salaam.
Dkt. Shekalaghe ameeleza kuwa lengo la kikao hicho ni kuwapitisha wadau katika mifumo mbalimbali ya rufaa inayotumika na watoa Huduma za Ustawi wa Jamii kutoka Serikalini na asasi za kiraia ili kutoka na maazimio ya nini kifanyike baada ya kikao kazi hicho.
“Kumekua na mifumo mbalimbali ya kutolea taarifa za Huduma za Ustawi ambazo hutolewa na vituo vinavyotoa huduma hizo vinavyoendeshwa na Serikali na asasi za kiraia hali ambayo imesababisha changamoto katika ufuatiliaji na kukamilika kwa huduma,” amesema Dkt. Shekalage
Dkt. Shekalage ameendelea kusema kuwa wajumbe katika kikao kazi hicho wanatarajia kuandaa nyaraka zitakazowezesha kupatikana kwa mwongozo wa mifumo wa rufaa kwa Makundi Maalum, kundaliwa kwa taratibu za utendaji za utoaji wa huduma (standard operating Procedures), kuandaa mfumo jumuishi wa rufaa wa kieletroniki, upatikanaji wa sera ya kuhifadhia takwimu za rufaa na huduma zinazotolewa kwa Makundi Maalum.
Aidha Makatibu Wakuu kutoka Wizara za kisekta kutoka Tanzania bara na Visiwani (Katibu Mkuu OR TAMISEMI, Katibu Mkuu WMJWW Zanzibar, Naibu Katibu Mkuu Mambo ya Ndani ya Nchi na Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya) wameahidi kutoa ushirikiano kwa Wizara katika kukamilisha uandaaji wa mfumo huo wa Kitaifa wa Rufaa.
Kikao hicho kimeandaliwa na Wizara kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uingereza na wadau wa Maendeleo UNDP kikiwa na lengo la kupata uelewa wa pamoja juu ya mfumo jumuishi wa Kitaifa wa rufaa.
0 Comments