UTAFITI WA VIASHIRIA NA MATOKEO YA UKIMWI KUZINDULIWA DISEMBA MWAKA HUU

Na Asha Mwakyonde,Dodoma

IDADI ya idadi ya maambukizi mapya inaendelea kupungua ikilinganishwa na matokeo ya Utafiti wa mwaka 2016/17 ambapo katika taarifa ya awali inaonesha Tanzania imepata Matokeo chanya katika Mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.

Uchakataji wa takwimu zilizokusanywa unaendelea na Taarifa ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya VVU na UKIMWI ya mwaka 2022/23 itazinduliwa rasmi Disemba1, 2023.  

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 31,2023 jijini Dodoma  na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama wakati akitoa taarifa kuhusu Kukamilika kwa utafiti wa Viashiria vya VVU na Ukimwi wa mwaka 2022/2023, alieleza kuwa hayo ni mafanikio mazuri ambayo Serikali ya Awamu ya Sita imeyafikia kuelekea kufikia Malengo ya kitaifa ya kufikia SIFURI TATU – yaani Kutokuwa na Maambukizi Mapya, Kutokuwa na Unyanyapaa na Ubaguzi, na Kutokuwa na Vifo Vitokanavyo na UKIMWI.


Waziri huyo amesema itakumbukwa kuwa, Serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya VVU na UKIMWI (Tanzania AIDS Impact Survey - THIS) kila baada ya miaka mitano.

Amesema  Utafiti wa mwisho ulifanyika mwaka 2016/17 lengo la utafiti huo ni Kupima matokeo ya juhudi za mapambano dhidi ya UKIMWI. Uzinduzi wa kuanza kwa Utafiti huu wa VVU na UKIMWI wa mwaka 2022/23 (THIS 2022/23) ulifanyika tarehe 29 Septemba, 2022 Jijini Mwanza. 

"Kupitia utafiti huu, tutapata taarifa kuhusu viashiria na matokeo ya VVU/UKIMWI katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka 2022/23 ambazo ni takwimu muhimu kuhusu hali ya UKIMWI nchini," ameeleza Waziri Mhagama.


Ameongeza kuwa utafiti wa mwaka 2022/2023 ni wa tano kufanyika nchini Tanzania, na wa pili wa aina ya Population Based HIV Impact Assessment - PHIA kufanyika katika ngazi ya Jamii. Tafiti za PHIA kwa mara ya kwanza zilifanyika nchini Tanzania mwaka 2016/17. 

Waziri huyo alibaisha kuwa tafiti za aina hiyo hufanyika kupima mwenendo wa VVU na UKIMWI Duniani, kwa kupima kiwango cha maambukizi mapya na Kufubaa kwa VVU katika ngazi ya jamii.

Amesema utafiti huo umefanywa  na Serikali ya Tanzania kupitia Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (Tanzania Commission for AIDS - TACAIDS), Tume ya Kudhibiti UKIMWI Zanzibar (Zanzibar AIDS Commission- ZAC), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (National Bureau of Statistics - NBS), Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar (Office of Chief Government Statistician - OCGS) kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za ndani na nje ya Serikali zikiwemo Kituo cha Kudhibiti Magonjwa na Kinga (Centre for Disease Control - CDC).


Pia utafiti huo ulifanywa na Chuo Kikuu cha Columbia (International Centre for AIDS Program I-CAP) kutoka nchini Marekani, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (National AIDS Control Program - NACP),na Mpango Jumuishi wa kupambana na UKIMWI, Homa ya Ini, Kifua Kikuu na Ukoma (Zanzibar Integrated HIV, Hepatitis, TB and Leprosy Program - ZIHHTLP). 

"Kazi hii imefanyika kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kudhibiti UKIMWI (Presidents Emergency Program for AIDS Relief- PEPFAR)," amesema Waziri Mhagama.

Amesema kwa kuwa wakati wa kuanza utafiti huo waliwapa taarifa, na kwamba waneona pia ni vyema Serikali ikawafahamisha kuwa Utafiti wa viashiria na matokeo ya VVU na UKIMWI umekamilika.

Aidha ametoa wito kwa wananchi kupokea taarifa hiyo ya awali na kujiandaa kupokea matokeo rasmi ya utafiti huu ifikapo Disemba Mosi, 2023. 

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI