DK.BITEKO: PURA KUNADI VITALU VYA UTAFUTAJI MAFUTA NA GESI ASILIA


Na Asha Mwakyonde Dodoma 

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA, inatarajia kuendesha Duru ya tano ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa lengo la kutangaza kwa wawekezaji vitalu vilivyo wazi katika eneo la bahari na nchi kavu. 

Pia Serikali kupitia PURA na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) iliendelea kusimamia na kudhibiti Sekta ya Nishati ili kuhakikisha utekelezaji wa shughuli za Sekta hiyo unazingatia sheria na taratibu zilizopo pamoja na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Hayo yamesemwa leo Aprili 24, 2024 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk.Doto Biteko wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka 2024/25 amesema kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na kuandaa nyaraka za zabuni zitakazoongoza mnada wa vitalu, kufanya maonesho ya kitaalamu kuhusu vivutio vya vitalu na kuzindua Duru ya tano ya kunadi vitalu. 

Amesema PURA iliendelea na maandalizi ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia kupitia Duru ya tano kwa kuandaa rasimu ya Mkataba Kifani wa Ugawanaji Mapato (Model Production Sharing Agreement-MPSA) wa mwaka, 2024 (MPSA, 2024) kwa ajili ya kutumika katika zoezi hilo na kukamilisha Mwongozo wa kupata kampuni za Kijiofizikia zitakazoshirikiana na Mamlaka hiyo katika zoezi la kunadi vitalu ambapo taratibu za kupata kampuni hizo zinaendelea.

"Ili kufikia azma ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wananufaika na uwekezaji katika rasilimali zilizopo katika maeneo yao,Serikali kupitia PURA na TPDC imeandaa rasimu ya Miongozo ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (Corporate Social Responsibility – CSR) katika Sekta Ndogo ya Mafuta na Gesi asilia inayotarajiwa kukamilika mwishoni mwa Juni, 2024," amesema .

Aidha, maandalizi ya rasimu yamehusisha wadau kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo mikoa ya Lindi na Mtwara.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI