TPDC : VIWANDA 57 NCHINI VINATUMIA GESI ASILIA, YAKARIBISHA WAWEKEZAJI UJENZI VITUO VYA GESI


Na Asha Mwakyonde, Dodoma 

MENEJA wa biashara ya Gesi Asilia kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),Mhandisi Emmanuel Gilbert ameeleza kuwa viwanda 57 nchini kutika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara,Lindi na Pwani vinatumia Gesi Asilia ambapo awali vilikuwa vinatumia mafuta mazito (Industrial Diesel).

Pia Mhandisi Gilbert amesema wanakaribisha sekta binafisi kwenda kuwekeza kwenye ujenzi wa vituo vya kujazia Gesi Asilia katika magari huku akisema tangu walivyofungua milango miaka mitatu iliyopita ya kuwakaribisha wawekezaji tayari vituo viwili vimeshajengwa.

Akizungumza jijini hapa leo Aprili 18,2024 katika Maonesho ya Wiki ya Nishati kwenye viwanja vya Bunge amesema kuwa TPDC wana mradi wa ujenzi wa vituo vya kujazia Gesi Asilia kwenye magari na kwa sasa tayari wameshapa mkandarasi wa kujenga kituo kimoja kikubwa jijini Dar es Salaam.

Mhandisi huyo amefafanua kuwa kituo hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kujaza Gesi Asilia ambapo yatajazwa magari 16 kwa wakati mmoja ambazo zitakuwa zimewekewa mfumo wa gesi hiyo.

Amesema kuwa wateja wao wamewaweka katika makundi tofauti ambapo kundi la kwanza ni la kuzalisha umeme na mteja wao mkubwa ni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),na kwamba kiasi wanachopeleka TANESCO kinaweza kuzalisha asilimia 60 ya umeme wote unaotumika hapa nchini unaozalishwa kutumia Gesi Asilia.

Mhandisi Gilbert amesema kuwa wanawateja wa viwanda ambao wanatumia Gesi Asilia kwa matumizi ya viwandani kama kuzalisha umeme wao wenyewe wa kuendeshea shughuli za viwanda na kutumia kama nishati ya kuchoma malighafi mbalimbali katika viwanda vyao badala ya kutumia nishati ya mafuta mazito au dizeli.

" Wanatumia Gesi Asilia kwanza ni bei rahisi lakini pia inatunza mazingira kwa kuwa ikichomwa inaungua kwa asilimia 100 na haitoi masinzi, hewa ukaa," amesema.

Ameongeza kuwa wateja wengine wamewaweka katika kundi la matumizi ya kupikia majumbani na baadhi ya taasisi ambazo zinatumia Gesi Asilia kama hotelini, vyuoni pamoja na magereza.

"Kwa mfano Mtwara tuna taasisi nne ambazo zinatumia Gesi Asilia gereza kuu la Lilungu, tumeonganisha nyumba zote za watumishi wa gereza, majiko ya jumuiya ya wafungwa yamehama katika kutumia kuni kwa ajili ya kupikia kwa sasa wanatumia Gesi Asilia pia tumeonganisha sekondari ya Ufundi Mtwara nayo inatumia gesi hii, chuo cha walimu Ufundi na kwa walimu wa kawaida," ameeleza.

Amesema kuwa eneo la nne wanapeleka kwenye vituo ambavyo vinaweza kutoa Gesi kwenye magari huku akifafanua kwamba gesi hiyo inaweza kutumika kuendeshea magari yanayotumia mafuta ya dizeli au petroli kwa kuwekewa mifumo maalumu zikabalishwa kutoka kwenye matumizi ya mafuta ikatimia gesi hiyo.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU