VIONGOZI BARAZA LA WAZEE WAPATIWA MAFUNZO MATUMIZI YA TAKWIMU, WATAKIWA KULINDWA, KUHESHIMIWA

Na Asha Mwakyonde, Dodoma 

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk.Dorothy Gwajima ameitaka jamii kuwapenda, kuwathamini na kuwalinda wazee dhidi ya vitendo vya ukatili, kuwaheshimu, kuwahudumiwa, kushirikishwa katika mipango ya kimaendeleo kutokana na ujuzi walionao ili kutumika katika kuchochea maadili chanya katika jamii. 

Dk. Gwajima amewataka Wazee nchini kuhakikisha wanayafahamu vyema matokeo ya Sensa na kuyatumia katika kuchagiza maendeleo ya taifa.

Waziri Dk. Gwajima ameyasema hayo leo Aprili 19,jijini hapa wakati akifungua mafunzo ya matumizi ya Matokeo Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kwa viongozi wa Mabaraza ya Ushauri ya Wazee Nchini amesema kuwa Serikali imefanikiwa kufanya mapitio ya Sera ya Wazee ya Mwaka 2003 ili iweze kuendana na mahitaji ya sasa ambapo mapitio ya Sera hii yameisha kamilika kwa hatua kubwa. 

Dk. Gwajima ameongeza kuwa tayari Sera imeshafikishwa kwenye vyombo mbalimbali vya maamuzi na sasa iko kwenye hatua za mwisho na kwamba wanaamini kuwa sera hiyo ikipitishwa na vyombo vya juu vya maamuzi itawapatia msingi mzuri wa kuanza mchakato wa maandalizi ya sheria ya wazee.

"Ninatambua kuwa bado kuna changamoto mbalimbali zinazo wakabili Wazee zinazotakiwa kufanyiwa kazi miongoni mwa changamoto hizi ni upatikanaji wa Sheria ya Wazee, Pensheni kwa Wazee wote na upatikanaji wa dawa za Wazee katika baadhi ya Vituo vya Afya," amesema Dk. Gwajima.

Dk. Gwajima ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kuwashughulikia ipasavyo wale wote watakaobainika kufanya vitendo vya ukatili kwa makundi mbalimbali katika jamii wakiwemo wazee.kushindikana. 

Aidha amewataka Viongozi wa mabaraza ya wazee kutumia Mabaraza hayo kujadili mambo ya ustawi wao huku akiwataka watoe kipaumbele kujadili mambo yanayohusu uzalendo na ujenzi wa maadili mema kwa watoto ili waweze kuwa na kizazi kilicho na dhamira ya dhati ya kuipenda nchi na kuitumikia.

Dk. Gwajima amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaenzi wazee kwa kwa kadri ya uwezo muda wote kupitia Wizara katika kushughulikia maslahi na ustawi wa wananchi na makundi maalum wakiwemo wazee.

Kamisaa wa Sensa nchini Anna Makinda ameeleza kuwa Taifa linawategemea Wazee hao katika kutengeneza maadili ya kizazi hiki katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwaandaa kuwa viongozi imara.

Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa amesema kuwa mafunzo hayo yanatokana na agizo la Rais Dk.Samia ambaye aliyazindua matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi mwaka ya mwaka 2022.

"Ofisi pia imeona umuhimu wa kuwapa mafunzo ili mfahamu matumizi ya matokeo na jinsi ya kuyatumia kwa sababu wazee ni tunu ya Taifa," ameeleza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Taifa Lameck Sendo amesema wazee wameridhika na hatua zote za maendeleo ya Taifa kwa kuhakikisha ustawi wa wazee hao unakuwa kuendana na kasi ya mabadiliko ya uchumi duniani.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI