WAZIRI MKUU AITAKA WIZARA YA NISHATI KUONDOA MLUNDIKANO WA MAOMBI KUUNGANISHIWA UMEME WANANCHI

Na Asha Mwakyonde,Dodoma 

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa ameitaka Wizara ya Nishati kuweka mkakati wa kuwawezesha wananchi wote kupata ufafanuzi na fursa zinazotokana na miradi inayotekelezwa katika Sekta ya Nishati.

Pia Waziri huyo ameitaka Wizara hiyo kusimamia na kuondoa mlundikano wa maombi ya kuunganisha umeme kwa wananchi na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ihakikishe inaimarisha mfumo wa kupokea maombi na kutekeleza maombi hayo kwa haraka.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Aprili 19, wakati akifunga Maonesho ya Wiki ya Nishati kwenye viwanja vya Bunge ameagiza Maonesho hayo yafanyike kuanzia ngazi ya wilaya, mikoa na halmashauri ili yale yanayofanyika Makao Makuu yabaki kuwa ya Kitaifa. 

Amefafanua kuwa kwa kufanya hivyo huduma zitakuwa zimesogezwa zaidi kwa kwa wananchi na pia Mameneja wa TANESCO wa Kanda, Mikoa na Wilaya watoe ufafanuzi wa hoja na changamoto zinazowakabili wananchi husika

"Maonesho haya yafanyike maeneo yanayofikika kwa urahisi kwa wananchi wengi kama katikati ya miji ili wananchi wengi washiriki na kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali, " Waziri Mkuu ameagiza.

Waziri Mkuu ameziagiza Taasisi zote zinazolisha watu wengi kuanzia 50 hadi 100 waanze kubadilisha teknolojia ya kupikia na kutumia Nishati Safi ya kupikia na ifikapo mwisho wa mwaka 2024 Serikali inataka kuona asilimia 99 ya Taasisi za aina hiyo zinatumia Nishati Safi ya Kupikia.

"Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa utendaji kazi wake ambao umechochea hali ya upatikanaji umeme nchini kuongezeka na kutosheleza mahitaji pamoja na kuwezesha upatikanaji wa umeme wa ziada," amesema.

Awali Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk.Doto Biteko amesema, wanafanyakazi kubwa kwa lengo la kubadilisha taswira ya hiyo na Taasisi zake huku akiwashukuru watendaji wa Wizara ya Nishati pamoja na Taasisi zake kwa kufanyakazi kwa juhudi ambapo amewaomba kuongeza kasi katika utendaji huo.

"Nilipongeza Shirika la TANESCO kwa kuendelea kuboresha utoaji huduma ya umeme nchini pamoja na wakandarasi wa umeme kwa kuendelea na utekelezaji wa miradi ya nishati katika maeneo mbalimbali nchini," amesema na kuongeza.

Navipongeza vyombo vya habari nchini kwa kuendelea kutangaza habari zinazohusu masuala ya nishati kwa lengo la kujibu hoja na maswali mbalimbali ya wananchi," ameeleza.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Tanzania Dk. Tulia Ackson, amesema mchango sekta ya umeme hauepukiki katika ngazi zote kuanzia vitongoji hadi Taifa huku sekra ya uzalishaji ikiwemo viwanda na migodi na maeneo mbalimbali ambapo amesisitiza umeme usitumike kwa ajili ya mahitaji ya awali pekee kama kuwasha taa na kuchaji simu.

Aidha Spika huyo ameishauri Serikali kuanzisha gridi ya maji kama ilivyo ya umeme ambayo ipo katika maeneo mengi nchini ili kusaidia usambazaji wa maji katika maeneo kame kwa kutumia gridi ya maji.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, David Mathayo

amesema Kamati yake itaendelea kushauriana na Wizara katika masuala mbalimbali yanayohusiana na nishati kama upelekeji wa huduma kwa wananchi wanaozunguka miradi hasa ya Gesi Asilia ili maisha yao yaendane na thamani ya miradi hiyo.

"Napongeza Wizara ya Nishati kwa kuandaa maonesho haya ambayo yametoa fursa kwa Wabunge na wananchi kupata uelewa kuhusu utekelezaji wa kazi zinazofanywa na Wizara hiyo pamoja na Taasisi zake na kushauri maonesho hayo kuwa endelevu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba ameeleza kuwa wabunge 267 wametembelea mabanda ya maonesho na kujionea kazi zinazofanywa na Wizara na Taasisi zake, kuuliza maswali na kutoa maoni na wananchi 213 walitembelea maonesho hayo

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI