Na Asha Mwakyonde,Dodoma
WAZIRI wa Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo ameeleza kuwa mambo matatu ya kufanya kukuza ustawi wa binadamu ni kumpa binadamu elimu ili aweze kuishi vizuri ambapo mwaka 2000 nchini, kiwango cha kuandikisha wanafunzi kilikuwa asilimia 69.
Haya ameyasema leo Aprili 17, 2024 jijini hapo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu miaka 60 ya Muungano na mafanikio ya wizara hiyo amesema malengo waliojiwekea kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025, ni kufikia asilimia 100 ya uandikishaji wa wanafunzi ambapo hadi sasa wamevuka malengo hayo ambapo wapo asilimia 108.5.
"Kuhusu suala la kwenda sekondari, mnamo mwaka 1964 ilikuwa asilimia 5, mnamo mwaka 2000, watoto waliofanikiwa kufika sekondari kutoka shule za msingi ilikuwa chini ya asilimia 20,Lengo la serikali ifikapo mwaka 2025, tuwe tumefika asilimia 48. Kwa takwimu za hivi sasa ambapo wapo asilimia 70," amesema na kuongeza.
Dira ya Maendeleo ya Taifa inayokuja, tutahitaji elimu ya msingi Tanzania iwe kwa Watanzania wote na wote lazima kufika sekondari kwa asilimia 100," ameeleza.
Waziri huyo amefafanua kuwa eneo la pili la kukuza ustawi wa binadamu ni afya hasa kwenye eneo la mama na mtoto, na la tatu ni maji ambapo wakati nchi inapata uhuru, uwepo wa maji vijijini ulikuwa chini ya asilimia 15 na mwaka 2000 ilikuwa asilimia 32 na kwa sasa ni asilimia 77.
Ameeleza kuwa nchi inahitaji uwepo wa uchumi, kukua kwa uchumi ni nyenzo muhimu na kwamba ili nchi ione inapiga hatua ni lazima iangalie uchumi unaendaje ambapo wakati wa Uhuru ilikuwa ni kilimo pekee .
Prof. Mkumbo amesema katika miaka takriban 20 iliyopita, uchumi wa nchi umekuwa ukikua vizuri kati ya wastani wa asilimia 6 mpaka 7 hivyo wanamengi ya kujivunia katika Muungano huku akisema wamefanikiwa kuzikabili na kuzitatua changamoto zilizojitokeza.
"Serikali imejidhatiti kupambana na changamoto zitakazojitokeza ambazo zitatishia muungano wetu,
tulipanga kupambana kuhakikisha kwamba muungano huu unadumu na tulipanga kulinda amani, utulivu na mshikamano hayo yote tumeyafanikisha. ameeleza Prof. Mkumbo.
Amesema wanapopima mafanikio kama nchi, wanazungumzia uhai wa taifa kama taifa hatua ya kwanza ya kupima katika miaka 60 ya muungano ni uhai wa muungano.
0 Comments