Na Asha Mwakyonde,Dodoma
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amesema,uzalishaji wa nyama umeongezeka kutoka tani 97,000 mwaka 1964 hadi tani 738,166 mwaka 2023 ambapo imetokana na kuongezeka kwa viwanda vya kusindika nyama kutoka kiwanda kimoja mwaka 1964 (Tanganyika Parkers) kilichokuwa na uwezo wa kuchinja ngombe 800 kwa siku hadi viwanda 11 vyenye uwezo wa kusindika tani 337 kwa siku.
Haya ameyasema leo Aprili 16, 2024 jijini hapa wakati akitoa taarifa ya mafanikio kuhusu Wizara hiyo katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya hivi karibuni, Mauzo ya nyama nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 1,774 mwaka 2020/21 hadi kufikia tani 14,701 mwaka 2022/23.
Alisema ongezeko hilo lina kufanya jumla ya tani 35,297 zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 146.43 zilizouzwa nje ya nchi.
Waziri huyo akizungumzia tasnia ya maziwa amesema uzalishaji wa maziwa umeongezeka kutoka lita 334,000 mwaka 1964 hadi lita bilioni 3.4 mwaka 2022/2023 na usindikaji wa maziwa umeongezeka kutoka wastani wa lita 41,026,000 kwa mwaka 1964 hadi wastani wa lita milioni 75.9 kwa mwaka 2023.
"Viwanda vya kusindika maziwa pia vimeongezeka kutoka viwanda saba vya umma mwaka 1974 hadi kufikia viwanda vya sekta binafsi 105 mwaka 2023," ameeleza Waziri Ulega.
Amesema Wizara imekuwa na ushirikiano na sekta binafsi katika kukuza sekta ya maziwa nchini. Kwa mfano Shirika la Heifer International limeweza kuimarisha mnyororo wa thamani kwa kuwapatia wafugaji wadogo kote nchini jumla ya mitamba bora wa maziwa 282,000, kuku 62,000 na kondoo 57,200 na kujenga vituo 22 vya kukusanyia maziwa vyenye uwezo wa kukusanya lita 70,000 za maziwa kwa siku.
Aidha Waziri Ulega amesema idadi ya wavuvi wadogo nayo imeongezeka katika kipindi cha mwaka 1961 hadi 1988 ambapo shughuli za uvuvi kwenye maeneo yote ya uvuvi nchini zilikuwa zikifanywa na wavuvi hao.
Waziri huyo ameongeza kuwa idadi hiyo imeongezeka kutoka wavuvi 75,621 mwaka 1995 waliokuwa wanatumia vyombo vya uvuvi 22,976 hadi wavuvi 198,475 waliotumia vyombo 58,820 mwaka 2023.
Waziri Ulega amesema, kiasi cha samaki kilichozalishwa na nguvu hiyo ya uvuvi (wavuvi na vyombo) kiliongezekakutoka tani 255,900.74 za samaki zenye thamani ya TShs. 70,467,575.96 mwaka 1995 hadi tani 479,976.6 zenye thamani ya shilingi trilioni 3.4 mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 87.56.
Kwa ujumla uzalishaji wa samaki umeonekana kuongezeka hali inayoashiria kuboreka kwa shughuli za uvuvi na maisha ya wavuvi wadogo nchini.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dk.Samia Suluhu Hassan, imewezesha utekelezaji wa mradi mkubwa wa kielelezo wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko wenye thamani ya shilingi bilioni 289.5 na tayari kiasi cha shilingi bilioni 106.23 kimetolewa.
"Ujenzi umefikia asilimia 52 na ajira za moja kwa moja 278 zimetolewa kwa wananchi katika eneo la mradi, ameeleza Waziri Ulega.
Alifafanua kuwa kukamilika kwa ujenzi huo kutawezesha Meli za uvuvi zinazovua katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari ya Tanzania (EEZ) na Bahari Kuu kutia nanga na kushusha samaki wanaolengwa na wale wasiolengwa, kuchochea uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki na miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya uvuvi, kuimarisha biashara ya mazao ya uvuvi kwenda nje ya nchi; na kuchangia katika pato la Taifa.
Waziri huyo amesema Sekta ya Mifugo ni miongoni wa Sekta za Kiuchumi na Uzalishaji ambayo inatoa ajira kwa wananchi wengi wa Tanzania, Sekta ya mifugo ilikua kwa asilimia 5.0 na mchango wa Sekta katika pato la Taifa (GDP) ulifikia asilimia 6.7 kwa mwaka 2022.
Amesema Idadi ya mifugo nchini ngombe milioni 36.6, mbuzi milioni 26.6 na kondoo milioni 9.1 ambapo kuku waliopo ni milioni 97.9 ambapo kuku wa asili ni milioni 45.1, kuku wa kisasa milioni 52.8 na nguruwe ni milioni 3.7.
0 Comments