Na Asha Mwakyonde,Dodoma
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni amesema Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu imefanikiwa kuokoa na kusaidia waathirika 1,338 waliokuwa wakitumikishwa ndani na nje ya nchi ambapo kati ya hao 1,211 waliokolewa hapa nchini na waathirika 127 walitoka nje ya nchi za Thailand,India,Oman, Yemeni, Kenya, Botswana, Malaysia na Iraq.
Akizungumza jijini hapa leo Aprili 15,2024 wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Jamhuri wa Tanzania Waziri Mhandisi Masauni amesema kati ya waathirika 1,338 waliookolewa 1,290 ni wanawake na 48 ni wanaume.
" Waathirika wote walipewa huduma muhimu zikiwamo malazi, matibabu, chakula, msaada wa kisheria ,urekebishaji na kuunganishwa na familia zao.
Pia Waziri Mhandisi Masauni ameeleza kuwa Sekretarieti hiyo imefanikiwa kufanya oparesheni za kusambaratisha mitandao inayojihusisha na usafirishaji haramu wa binadamu ambapo kupitia oparesheni hizo wahalifu 218 walikamatwa na kesi 131 zilifunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini.
Amefafanua kuwa kati ya kesi hizo 107 zimeshatolewa uamuzi na wahalifu 81 walipatikana na hatia ambapo walipewa adhabu ikiwamo kifungo gerezani.
"Wizara kupitia Sekretarieti imefanikiwa kuanzisha Ofisi ya Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu -Zanzibar ili kuimarisha mapambano dhidi ya biashara haramu ya usafirishaji haramu wa binadamu," amesema Waziri, Mhandisi Masauni.
Ameongeza kuwa Wizara hiyo kupitia Sekretarieti imefanikiwa kuanzisha Mfuko wa Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu ( The Ant- Trafficking Fund), ili kuimarisha huduma zitolewazo kwa waathirika hao.
Waziri, Mhandisi Masauni ameeleza mfuko huo ni mahsusi kwa ajili ya kusaidia waathirika tu na unapata fedha kutoka serikalini na kwa wadau mbalimbali wakiwamo watu binafisi ambapo umeenzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Usafirishaji Haramu wa Binadamu Namba 6/2008.
0 Comments