WAZIRI SIMBACHAWENE: MAFANIKIO YAMEPATIKANA KUPITIA MUUNGANO ENEO LA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA


Na Asha Mwakyonde, Dodoma 

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Utumishi na Utawala Bora George Simbachawe amesema kuwa katika kipindi hiki cha miaka 60 ya Muungano, wameona na kushuhudia wazi mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kupitia Muungano katika eneo la Utumishi wa Umma na Utawala Bora. 

Pia amesema kuwa idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Tanzania Bara inashirikiana na Idara ya Nyaraka na Kumbukumbu-Zanzibar kuweka mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu za Kiutendaji katika baadhi ya Wizara za Serikali ya mapinduzi Zanzibar.

Hayo ameyaeleza leo Aprili 15, 2024, Jijini hapa  alipokuwa akitoa Taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka 60 ya Muungano kwenye eneo la utumishi wa umma na utawala bora. 

Amesema  Mafanikio hayo yanatokana na azma ya Waasisi wa Taifa hili pamoja na Viongozi Wakuu wa Serikali zote mbili wa sasa yaani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi kwa kuboresha na kuuendeleza ushirikiano ulioanzishwa na Waasisi Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.

Simbachawene amewashukuru na kuwapongeza kwa dhati Viongozi hao  kwa kudumisha muungano katika kipindi hicho cha miaka 60, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mujibu wa Hati Idhini ambayo imeainisha mgawanyo wa majukumu Serikalini.

Ameongeza kuwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ina majukumu ya 

Kusimamia uendelezaji sera katika Utumishi wa Umma, Utawala wa Utumishi wa Umma, Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Mishahara, Usimamizi wa Mifumo ya Uendeshaji wa Serikali, Usimamizi wa Mifumo ya Utendaji Kazi wa kila Siku Serikalini, Uendelezaji Rasilimaliwatu, Ukuzaji wa Maadili katika Utumishi wa Umma, Usimamizi wa Serikali Mtandao na Usimamizi wa Anuai za Jamii katika Utumishi wa Umma,

"Ofisi hii  ina dhamana ya kusimamia masuala ya Utawala Bora na Vilevile ina jukumu la kusimamia taasisi fungamanishi zinazoshiriki katika kuleta maendeleo na ustawi wa wananchi nchini,"ameeleza.

Amesema kuwa Muungano umeendelea kuimarishwa kupitia Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Tanzania Bara na Idara ya Nyaraka na Kumbukumbu-Zanzibar ambapo kwa pamoja wanaratibu, kuandaa na kushiriki katika makongamano ya kuwaenzi Waasisi wa Taifa (Mwl. Julius K. Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume).

Waziri Simbachawene amefafanua kuwa Idara hizo zinashiriki kwa pamoja kwenye mikutano ya vyama vya Kitaalam vya Kitaifa na Kimataifa vinavyohusika na masuala ya utunzaji na uhifadhi wa kumbukumbu na nyaraka kama vile; Eastern and Southern Africa Branch of the International Council on Archives (ESARBICA) na International Council on Archives (ICA); Chama cha Watalaam wa Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA),

Amesema Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Tanzania Bara inashirikiana pia na Idara ya Nyaraka na Kumbukumbu-Zanzibar kufanya ziara za kimafunzo ili kubadilishana uzoefu na utalaamu katika utunzaji na uhifadhi wa kumbukumbu na nyaraka kati ya taasisi zenye dhamana na uhifadhi na menejimenti ya kumbukumbu na nyaraka.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU