CHUO CHA NIT KUANZA KUTOA MAFUNZO YA URUBANI SEPTEMBA MWAKA HUU

Na Asha Mwakyonde,Dodoma 

WAZIRI wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali imekamilisha ununuzi wa Ndege mbili za injini moja za mafunzo ya urubani na taratibu za kuanza Mafunzo ya Urubani katikaChuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), zinaendelea ambapo mafunzo yanatarajiwa kuanza mwishoni mwa Septemba, 2024.

Akiwasilisha hotuba yake ya Mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25 bungeni leo Mei 6, 2024 Jijini Dodoma, Waziri wa Uchukuzi Prof. Mbarawa amesema kuanza kutolewa mafunzo hayo hapa nchini kutapunguza gharama na kuongeza wigo na fursa kwa Watanzania kusomea mafunzo ya Urubani.

Waziri huyo amesema serikali kupitia NIT imeendelea kutekeleza mradi wa kuboresha miundombinu na vifaa vya kufundishia ambapo ujenzi wa Kituo cha Raslimali Mafunzo(Maktaba) umefikia asilimia 75; uundwaji wa Ndege moja yenye injini mbili kwa ajili ya kufundishia Marubani unaendelea kiwandani nchini Marekani na unatarajiwa kukamilika Machi 2025. 

Prof. Mbarawa ameeleza kuwa zoezi la kukamilisha upembuzi yakinifu kwa ajili ya uanzishwaji wa Kituo Atamizi cha Mafunzo (Incubation Centre), ya wataalam mahiri wa Usafiri Majini Mkoani Lindi lipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji.

Ameongeza kuwa Chuo cha NIT kupitia Kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya Taaluma za Usafiri wa Anga na Operesheni za Usafirishaji kilichoanzishwa chini ya Mradi wa East Africa Skills for Transformation and Regional Intergration Project (EASTRIP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kimeendelea kutekeleza kazi za mradi zikiwamo ujenzi wa majengo matano yanayojengwa katika Kampasi ya Mabibo – Dar es Salaam ambayo yana madarasa 11, maabara 16, karakana tano (5), mabweni ya wanafunzi mawili (2) na ofisi za watumishi 13, ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 75.

Kwa mujibu wa Prof. Mbarawa Ujenzi wa majengo matatu katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) ambayo ni Karakana ya Matengenezo ya Ndege (Aviation Hangar), Bweni la wanafunzi 20 wa Urubani na nyumba za watumishi 10 upo katika hatua ya ununuzi wa mkandarasi na ununuzi wa Vifaa vya mafunzo ya Urubani na Uhandisi Matengenezo ya Ndege ikiwemo Flight Simulators mbili (2), Workshop, Multimedia and Computer Based equipment umefikia asilimia 60.

Amesema Chuo cha NIT kupitia Kituo cha Kikanda cha Umahiri cha Mafunzo ya Usalama Barabarani kilichoanzishwa kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kimeendelea kutekeleza kazi zake za ufungaji wa vifaa vya TEHAMA ikiwemo Camera with ZOOM, Digital Television, CCTV Cameras, WiFi AP and Teleconferencing System kwa ajili ya mafunzo ya usalama barabarani upo kwenye hatua za mwisho.

Waziri huyo amefafanua kuwa kukamilisha uandaaji miongozo 16 ya kufundishia ambao umesaidia kuboresha utoaji wa mafunzo katika Chuo cha NIT, Mafunzo ya kozi ya Ukaguzi wa Usalama Barabarani yamefanyika kwa washiriki 180 katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini katika mkoa wa Njombe 23, Kanda ya Kati Dodoma 26, Kanda ya Ziwa - Mwanza 58 na Zanzibar 7.

Amesema taarifa ya awali (Inception report) kwa ajili ya uandaaji wa mitaala na miongozo ya kuwajengea uwezo watumishi katika kufanya tafiti na kutoa ushauri elekezi katika masuala ya usalama barabarani imeandaliwa na kukamilika.

"Katika kuendelea kuboresha utoaji wa huduma ya elimu na mafunzo kwa ufanisi zaidi, Chuo cha NIT kimeendelea kuwajengea uwezo watumishi katika mafunzo ya muda mrefu ambapo jumla ya watumishi 78 wanaendelea na mafunzo haya," ameeleza. 

Amesema kati ya watumishi hao 41 wanasoma Shahada ya Uzamivu, 26 Shahada ya Uzamili, watano mafunzo ya Urubani (Integrated Commercial Pilot License Course - ICPL) na watumishi sita mafunzo ya Leseni ya Matengenezo ya Ndege (Basic Aircraft Maintenance Technician License).

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI