PROF. MBARAWA: TASAC KUKUSANYA BILIONI 82.85 KUTOKA VYANZO VYA NDANI MWAKA WA FEDHA 2024/2025


Na Asha Mwakyonde, Dodoma 

SERIKALI kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC),imesema kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 imeweka lengo la kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 82.85 kutoka katika vyanzo vya mapato vya ndani. 

Akiwasilisha hutuba yake ya Mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25 jana bungeni Jijini Dodoma Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na kutoa leseni kwa watoa huduma zinazodhibitiwa na kusimamia masharti ya leseni, kudhibiti nauli na tozo mbalimbali za usafiri majini kwa kuzingatia Sheria na kanuni ili kuhakikisha kuwa tozo hizo zinaendana na gharama za uzalishaji na pia zinaleta ushindani katika soko.

Waziri huyo amesema kazi nyingine ni kufanya ukaguzi wa meli za nje zinazokuja katika bandari za Tanzania Bara na meli zilizosajiliwa nchini ili kuhakikisha vyombo hivyo vinazingatia viwango vya ubora, usalama na utunzaji wa mazingira ,kuongeza vifaa na kuratibu kazi za utafutaji na uokoaji sambamba na mazoezi ya utafutaji na uokoaji majini, kuimarisha mifumo ya utoaji wa Vyeti vya Mabaharia.

"Kuweka mifumo thabiti ya kukabiliana na uchafuzi wa mazingira majini utokanao na meli ,kuimarisha uratibu wa shughuli za kukabiliana na matukio ya meli kuvujisha mafuta baharini, kutoa elimu na uelewa wa masuala yanayohusu usalama, ulinzi na udhibiti wa uchafuzi wa mazingira utokanao na meli," ameeleza.

Prof. Mbarawa ameongeza kuwa kazi nyingine ni kuendelea kutoa huduma za uwakala wa forodha zinazojumuisha ugomboaji na uondoshaji wa bidhaa mahsusi, ambazo ni silaha na vilipuzi, makinikia, wanyama hai kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Wanyamapori, nyara za Serikali na kemikali zinazotumiwa na kampuni za madini,kuendelea kuimarisha mifumo ya mapato na matumizi kwa kukuza matumizi ya TEHAMA katika kudhibiti huduma za usafiri na biashara ya usafirishaji majini.

Amesema serikali itaendelea kuandaa kanuni na nyenzo za utendaji zitoazo mwongozo kuhusu udhibiti huduma za usafiri majini, usalama na ulinzi kwa vyombo vya usafiri majini na uchafuzi baharini kutoka katika meli, kuendelea kusimamia utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa kuhusu Usafirishaji majini inayoratibiwa na Shirika la Bahari Duniani (International Maritime Organization).

Pia ameeleza kuwa kazi hizo ni pamoja na kuendelea kuwajengea uwezo watumishi katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na shughuli za udhibiti ili kuendelea kukidhi haja na kukabiliana na changamoto za kupanuka kwa maeneo ya udhibiti na mabadiliko ya teknolojia na

kuendelela kutoa huduma na elimu kwa Watumishi kuhusiana na masuala mtambuka kama vile UKIMWI na rushwa na elimu kwa umma kuhusu sekta zinazodhibitiwa na Shirika kwa kupitia njia mbalimbali kama vile redio, runinga, magazeti, vipeperushi, mikutano ya wadau, maonesho na mitandao ya kijamii.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI