KIKKIDES AWATAKA VIJANA KULINDA AMANI, AONYA KUHADAIWA NA MITANDAO


Na Mwandishi Wetu

MRATIBU wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), ambaye pia ni Balozi wa Amani wa Taasisi ya Wanawake Nchini Korea Kusini, Fatma Fredrick Kikkides, amewataka vijana nchini kulinda amani iliyopo na kuepuka kudanganyika kwa kufuata mikumbo ya mitandaoni.

Kikkides alitoa wito huo Oktoba 23, 2024, kupitia mahojiano maalum aliyofanya na Televisheni ya Taifa (TBC2), ambapo alisisitiza umuhimu wa vijana kutambua nafasi yao katika kuimarisha amani ya Taifa.

“Vijana ndio nguzo ya Taifa, ni nguvu kazi kubwa inayotegemewa. Hivyo, ni jukumu lenu kulinda amani tuliyonayo na kuikabidhi kwa vizazi vijavyo. Amani inaanzia kwenye nafsi, nyumbani na hata kazini,” alisema Kikkides.

Aidha, aliwahimiza vijana kutambua thamani ya amani na kujiepusha na makundi yenye misimamo mibaya yanayotumia mitandao ya kijamii kueneza chuki na uvunjifu wa amani.

“Msikubali kushawishiwa na watu wasiokuwa na nia njema na nchi yetu. Wapo wanaotumia mitandao kueneza taharuki na kuharibu amani, lakini ni jukumu lenu vijana kujitambua na kusimama kidete kuitetea nchi yenu,” aliongeza.

Kikkides pia alibainisha kuwa changamoto kubwa kwa vijana wengi ni ukosefu wa elimu ya kutambua maana na thamani ya amani, jambo linalowasukuma kujiunga na makundi mabaya kwa hasira za ukosefu wa ajira.

 “Tunapaswa kuwajengea vijana uelewa juu ya amani. Wengi wanapotea kutokana na kukata tamaa, lakini ni lazima watambue kuwa amani ni urithi wa thamani mkubwa kuliko chochote,” alisisitiza.

Post a Comment

0 Comments

KIKKIDES AWATAKA VIJANA KULINDA AMANI, AONYA KUHADAIWA NA MITANDAO