DODOMA
NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amewataka Waumini kuliombea Taifa na kushiriki kupiga kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 29 Oktoba, 2025.
Mpanju amesema hayo leo 26 Oktoba 2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na waumini wa Kanisa la Pentekoste Assemblies of God Tanzania, katika tukio la ugemaji rasilimali fedha kwa ajili ya ujenzi wa darasa la watoto kanisani hapo.
Wakili Mpanju amesema jukumu la kanisa ni kuombea Taifa na ni wajibu wa kila raia kutimiza haki ya msingi ya kikatiba ya kuchagua viongozi watakaotumikia Taifa katika majira mapya.
“Amani ya Taifa lolote inakuwepo pale ambapo raia wake wanaombea nchi pamoja na wao kutimiza wajibu wao wa kisheria na kikatiba, hivyo niwaombe waumini wa kanisa hili popote walipo Tanzania muende mkashiriki kupiga kura na kuendelea kuombea Uchaguzi ufanyike kwa amani na utulivu” amesisitiza Wakili Mpanju
Aidha Wakili Mpanju ameupongeza Uongozi wa Kanisa hilo kwa kuwa na maono ya kujenga darasa la watoto kwa kusema kuwa jambo hilo litaimarisha malezi ya watoto kiroho na kimwili na kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, yenye dhamana ya kusimamia malezi na makuzi ya awali ya watoto, itaendelea kushirikiana na taasisi za kidini zenye maono yanayolandana na azma ya Serikali.
Katika zoezi hilo la ugemaji rasilimali fedha Wakili Mpanju pamoja na marafiki zake ameahidi mchango wa shilingi milioni ishirini.
Awali akisoma Risala Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Pentekoste Assemblies of God Tanzania, Dkt. James Kisanta amesema maono ya Kanisa hilo ni kuendelea kutoa huduma za kiroho na kijamii na kwamba mpango wa muda mrefu ni kujenga shule ya watoto wadogo mchana, kituo cha afya na chuo cha mafunzo ya ufundi stadi ili kusaidia kukuza utoaji wa huduma na maendeleo ya kijamii.




0 Comments