WIZARA YA ELIMU YAOMBA ZAIDI YA TRILIONI 1.9, YAANIKA VIPAUMBELE VYAKE 2024/2025


Na Asha Mwakyonde, Dodoma 

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeliomba Bunge kuidhinisha zaidi ya Shilingi Trilioni 1.9 ili kuwezesha wizara hiyo katika utekelezaji wa malengo yake kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Pia katika mwaka wa fedha 2024/2025, Wizara hiyo imepanga kutekeleza vipaumbele vitano vyenye lengo la kuongeza ubora wa elimu kwa kuwezesha vijana wa Kitanzania kupata maarifa, ujuzi, kujiamini, kujiajiri na kuajirika.

Akiwasilisha hotuba yake ya Mpango na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/2025 leo Mei 7, 2024 bungeni Jijini Dodoma, Waziri wa wizara hiyo Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa vipaumbele hivyo ni vyenye kujielekeza katika kutegemeza tafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu katika agenda ya maendeleo ya nchi.

Waziri Prof. Mkenda amevitaja vipaumbele hivyo vya mwaka wa fedha 2024/2025 kuwa ni kuendelea na utekelezaji wa sera na mitaala, mapitio ya sheria na kuandaa miongozo ya utoaji elimu na mafunzo nchini, kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (amali na amali sanifu).

Prof. Mkenda amesema vingine ni kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya msingi, sekondari na ualimu, kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya juu na kuendeleza tafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu.

Akizungumzia kuendelea na utekelezaji wa Sera na Mitaala, Mapitio ya Sheria na kuandaa Miongozo ya Utoaji Elimu na Mafunzo Nchini amesema Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 na Mitaala kwa ngazi ya Elimu ya Msingi, Sekondari na Ualimu.

Prof. Mkenda ameongeza kuwa wizara itaendelea na uandaaji wa zana za utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 ambazo ni Miongozo, Mfumo wa Kitaifa wa Tuzo na Sifa Linganifu (Tanzania Qualification Framework TQF), Sheria na Kanuni, Mfumo wa Mtaala wa Kitaifa na Mfumo wa Tathmini wa Kitaifa katika ngazi ya Elimu ya Msingi, Sekondari, Ualimu, Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Elimu ya Juu kwa lengo la kuwezesha ufanisi katika utekelezaji wa Sera.

"Serikali itaendelea na maboresho ya mitaala ya elimu ya amali sanifu na elimu ya juu ili kuwezesha nchi kuandaa rasilimaliwatu yenye ujuzi na maarifa, ameeleza Waziri huyo.

Ameeleza kuwa ktika kufikia azma hiyo, Serikali itatekeleza yafuatayo kufanya mapitio ya mitaala 171, kuandaa mitaala mipya 18, kuanzisha programu za vipaumbele 145 pamoja na matumizi ya mbinu bunifu za ufundishaji katika elimu ya juu.

Amesema Serikali itawezesha ziara za kimkakati kwa wafanyakazi wa sekta ya elimu katika nchi zenye uzoefu wa uandaaji wa rasilimaliwatu yenye maarifa na ujuzi wenye kuchangia katika ukuaji wa kati wa uchumi, na kwamba itasasisha na kuandaa mtaala mpya katika taasisi 17 za elimu ya juu pamoja na kuhakiki mitaala 230 ya vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.

Prof. Mkenda amefafanua kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa mafunzo yanayotolewa yanakidhi mipango ya nchi, soko la ajira la kitaifa na kimataifa na kuwawezesha wahitimu kujiajiri na kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira.

Amesema Serikali itaendelea kutoa elimu kuhusu maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 kwa watendaji wa ngazi zote za elimu na mafunzo wakiwemo walimu wa shule za msingi; walimu wa shule za sekondari, wakufunzi wa vyuo vya ualimu, wakufunzi wa vyuo vya ufundi, wakufunzi wa vyuo vya VETA,wakufunzi wa vyuo vya maendeleo ya wananchi,maafisa elimu msingi, maafisa elimu sekondari, wasimamizi wa elimu ngazi ya mkoa; maafisa elimu kata, wathibiti ubora wa shule, na wanataaluma kutoka taasisi za elimu ya juu. 

Waziri huyo amebainisha kuwa serikali itaendelea kutoa mafunzo kazini kwa walimu wa shule za msingi na sekondari kuhusu mitaala iliyoboreshwa na kwamba itaendelea na mapitio ya Sheria ya Elimu, Sura 353 ili iendane na Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023. 

MAPITIO YA SERA 

Prof. Mkenda ameeleza kuwa serikali itafanya mapitio ya sharia na miundo ya taasisi mbalimbali zikiwamo Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH),Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB),Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi(VETA),Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

Amesema taasisi nyingine ni Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET,)TIE, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima(TEWW),na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), ili ziendane na maboresho ya Sera na Sheria na makuliano mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa.

Waziri huyo amesema Kupitia wizara hiyo itafanya marekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mikopo kwa lengo la kuongeza ufasini wake ikiwamo kurahisisha ufunguaji wa mashauri na utekelezaji wake.

Ameongeza kuwa serikali itaendelea kuhuisha miongozo mbalimbali ya utoaji elimu na mafunzo nchini ili kuendana na maboresho ya Mitaala na Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 kama kukamilisha Mwongozo wa Kuwatambua na Kuwaendeleza Wanafunzi wenye Vipawa na Vipaji pamoja na kuandaa Mwongozo wa Elimu Jumuishi wa Ufundishaji na Matumizi ya Teknolojia kwa lengo la kuongeza ufanisi katika ufundishaji na matumizi ya teknolojia katika elimu na mafunzo.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI