Na Asha Mwakyonde, Dodoma
MBUNGE Viti maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Rukwa Bupe Mwakang’ata ameiuliza serikali,je ina mpango gani wa kukamilisha mradi wa maji kutoka Ziwa Tangayika na kusambaza maji katika Mkoa wa Rukwa?
Bupa ameuliza swali hilo la msingi leo Mei 9,2024 bungeni jijini hapa katika kipindi cha maswali na majibu.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa katika kuhakikisha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira inaimarika katika Mkoa wa Rukwa, Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu wa awali wa kutumia chanzo cha Ziwa Tanganyika ambacho ni cha uhakika.
Naibu Waziri huyo ameeleza kuwa hadi sasa, taratibu za manunuzi za kumpata mtaalam mshauri wa usanifu wa kina wa kutoa maji Ziwa Tanganyika na kuyapeleka katika mikoa ya Rukwa, Katavi mpaka Kigoma zimeanza na zitakamilika mwaka 2024/2025.
Mbunge huyo akiuliza maswali ya nyongeza amesema kuwa anashukuru kwa majibu mazuri ya serikali huku akiuliza,kwa kuwa Wilaya ya Nkasi inachagamoto ya maji je serikali inampango gani wa kupeleka mpango wa dharura ikiwamo kuchimba visima na mabwawa ?
Katika swali lake la pili mbunge huyu ameiuliza serikali ni lini mradi wa Isale utakamilika?
Akijibu maswali hayo Naibu Waziri huyo amesema"Kwanza nimpongeze mheshimiwa mbunge kwa kuwapigania wananchi wa Mkoa wa Rukwa katika miradi yetu ya maji na hakika tutaendelea kushirikiana nae kuhakikisha tunatatua changamoto za maji," ameeleza.
Amesema mpango wa serikali wa muda mfupi ,kati na mrefu kwamba mradi unaoendelea ni wa muda mrefu ambao bado wana changamoto ambapo Serikali inachimba visima vitatu vya maji vitakavyoenda kutatua tatizo la maji.
Naibu Waziri huyo ameeleza kuwa wanavisima vingine vitatu ambavyo wanaenda kuvichimba katika mwaka wa fedha 2024/2025 na kwamba vinatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha ujao.
Mhandisi Kundo amemhakikishia mbunge huyu kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha wananchi wake wanapata maji safi na salama.
Katika swali la pili ameeleza kuwa mradi wa Isale hadi sasa umefikia asilimia 75 ya utelelezaji wake na kwamba unagharimu takribani milioni 643 ambapo tayari serikali imeshamlipa mkandarasi milioni 262 ambapo wanaamini mkandarasi ataendelea na kasi ile ile ili akamilishe mradi huo.
0 Comments