Na Asha Mwakyonde,Dodoma
SERIKALI imesema kupitia maboresho ya mifumo ya usajili wa kimtandao yanayoendelea kufanyika hadi kufikia Machi, 2024, katika kusajili Kampuni, Majina ya biashara, Alama za Biashara, Huduma, Hataza na vyeti vya Viwanda ambapo Wizara ya Viwanda na Biashara imefanikiwa kusajili jumla ya Makampuni 10,651 kati ya 15,000 yaliyokusudiwa sawa na asilimia 71.
Akiwasilisha hotuba yake ya Mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2024/2025 leo Mei 21,2024 bungeni Jijini hapa Waziri wa wizara hiyo Dk.Ashatu Kijaji amesema imesajili Majina ya Biashara 19,040 kati ya 28,000 yaliyopangwa, sawa na asilimia 68, kusajili Alama za Biashara na Huduma 1,998 kati ya 4,200 zilizokuwa zimepangwa, sawa na asilimia 48 na kupokea na kuchakata maombi ya Hataza 45 kati ya maombi 40 yaliyokuwa yamepangwa sawa na asilimia 125 ya lengo lililowekwa.
Waziri huyo ameeleza kuwa hatua hizo zimetokana na juhudi kubwa za kutoa elimu kwa Umma kuhusu umuhimu wa kurasimisha biashara kupitia matamasha, warsha, maadhimisho na makongamano mbalimbali nchini.
Akizungumzia kuhusu kutoa Leseni na Kufanya Kaguzi Elimishi za Leseni za Biashara kundi ‘A’ na za Viwanda amesema hadi kufikia Machi, 2024, Wizara imefanikiwa kutoa Leseni za Viwanda 159 kati ya leseni 210 zilizokuwa zimepangwa sawa na asilimia 73.
"Wizara imetoa Leseni za Biashara kundi “A’’ 12,501 kati ya leseni 14,000 zilizopangwa sawa na asilimia 89, matokeo hayo yanatokana na jitihada za Serikali katika kusimamia na kudhibiti taratibu za ufanyaji wa biashara unaozingatia sheria," amesema.
Dk. Kijaji ameongeza kwamba hadi kufikia Machi, 2024, Wizara imefanya jumla ya kaguzi elimishi nne (4) za Viwanda na Leseni za Biashara katika Mikoa ya Manyara, Iringa, Simiyu na Kigoma ambapo elimu kuhusu Sheria ya Leseni na Usajili wa Viwanda vya Taifa, Sura ya 46 na Sheria ya Leseni za Biashara Na. 25 ya Mwaka 1972 imetolewa.
Amefafanua kuwa kumla ya biashara 728 zilikaguliwa ambapo kati ya hizo, biashara 471 zilikuwa na leseni halali za biashara, biashara 177 hazikuwa na leseni ya biashara, biashara 48 zilikuwa na leseni za biashara zilizoisha muda na biashara 32 zilikuwa na leseni za biashara kundi ‘B’ badala ya kundi ‘A’.
Waziri huyo ameeleza kwa upande wa Leseni za Viwanda jumla ya viwanda 333 vilikaguliwa ambapo kati ya hivyo,viwanda 46 vilikuwa na leseni, viwanda 279 havikuwa na leseni na viwanda 8 havifanyi kazi.
Amesema hatua zilizochukuliwa kwa viwanda ambavyo havina leseni za viwanda ni pamoja na Kuwaelekeza wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda waliokuwa hawana leseni kuomba leseni kwenye Mamlaka husika, kuhuisha leseni zilizoisha muda wake, na kuwaelekeza kuomba leseni papo kwa papo.
Waziri Dk. Kijaji amesema hatua nyingine ni pamoja na kutoa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kufanya biashara kwa kufuata Sheria za Nchi, kuzikumbusha Halmashauri kuhusu uzingatiaji wa Jedwali la Aina za Biashara na Ada katika utoaji wa Leseni za Biashara ili kutoingilia kundi la Mamlaka nyingine kuwakumbusha wamiliki wa viwanda kuwasilisha taarifa za maendeleo ya viwanda kwa kuwa taarifa hizo ni hitaji la kisheria.
Amesema elimu kuhusu mifumo ya kielektroniki inayotumika katika kutoa leseni za viwanda na leseni za biashara kundi “A” kwa njia ya mtandao ilitolewa kwa jumla ya wafanyabiashara 1,061 katika maeneo mbalimbali ya nchi.
"Wizara imekamilisha taratibu za kisheria kwa ajili ya kutoa msamaha wa ada ya kuwasilisha nyaraka za kampuni nje ya muda kwa kampuni zilizosajiliwa kabla ya mwaka 2018 ambazo taarifa zake hazijajumuishwa kwenye Mfumo wa Usajili wa Kampuni kwa njia ya Mtandao," ameeleza.
Amesema lengo la uamuzi huo ni kutoa unafuu wa ada kwa kiwango cha 50% ili kuwezesha kampuni hizo kuhuisha taarifa zao kwenye Mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao.
0 Comments