KINA MAMA EPUKENI MIKOPO UMIZA- MHE. NDERIANANGA


Na Mwandishi wetu- KILIMANJARO

Mbunge wa Viti Maalum ambaye pia ni NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Ummy Nderiananga amewataka Wakinamama kuachana na mikopo umiza (kausha damu) na badala yake watumie mikopo inayotolewa na Serikali kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya kila Halmashauri.

Naibu Waziri Ummy ametoa kauli hiyo alipofanya ziara ya kuzungumza na Viongozi wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Tarafa ya Mamba vunta, Gonja na Ndungu na badae kufanya mkutano wa hadhara kata ya Maore wilayani Same mkoani Kilimanjaro.

Alisema kuwa, mikopo hiyo ambayo ni asilimia nne wanawake na vijana huku watu wenye ulemavu ikiwa ni  asilimia mbili iliyositishwa  na serikali kwa lengo la  kuwekewa utaratibu mzuri ambapo kwa sasa itaanza kutolewa baada ya utaratibu wake kukamilika.

"Wakinamama tumekuwa tukiumizwa sana na hii mikopo umiza ambayo ni kausha damu huku wengine  ndoa zetu zikivunjika  kutokana na mikopo hiyo huku wengine  tumekuwa tukikimbia familia zetu sasa Serikali imerejesha mikopo hivyo tuachane na mikopo umiza tuchukue hii ya Serikali tujinufaishe," Alisema Naibu Waziri Ummy.

Aidha kiongozi huyo alisema kuwa, serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya miradi mikubwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Wilaya ya Same huku akiwahimiza wananchi kuiunga mkono Seraikali ili iendelee kuleta maendeleo zaidi katika maeneo yao.

Akiwa katika mkutano wa hadhara, Naibu Waziri Ummy aliwahamasisha wananchi wakiwemo watu wenye ulemavu kushiriki kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili kutumia haki yao ya kikatiba kuwachagua viongozi Bora watakaowaongoza kwa kipindi cha miaka mitano huku akitoa msaada wa kiti mwendo kwa mtu mwenye ulemavu katika Tarafa ya Gonja.

Awali Diwani wa Kata ya Maore, Issa Rashidi alisema kuwa, Kata hiyo ilikuwa upinzani kwa miaka mitano lakini mwaka 2020 wananchi waliamua kufanya maamuzi na kuwachagua viongozi wanaotokana na CCM ambapo ipo miradi mikubwa imetekelezwa.

“ Mwaka 2023, Wanafunzi 500 waliohitimu darasa la saba walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ambapo Kata hii ina shule mbili za sekondari na kupelekea kuwa na mrundikano wa wanafunzi hivyo tunaiomba Serikali chini ya Rais wetu msikivu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan itusaidie kujenga  shule nyingine ya sekondari katika eneo hili ili kupunguza mrundikano wa wanafunzi darasani,”Alieleza Diwani Huyo.

Aidha Diwani huyo alisema kuwa, mbali na mafanikio yaliyopo katika Kata hiyo lakini wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji ya kutosha kwa wananchi ambapo hadi sasa wamefanikiwa kupata mradi wa maji wa Mbuta huku akiwataka wakandarasi kuongeza  kasi ya ujenzi wa mradi huo  ili wananchi waweze kuondokana na kero ya maji.

Naye Afisa Tarafa, Kata ya Ndungu, Kalua Mhunzi aliipongeza Seraikali kwa kuendelea kujenga miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujeniz wa Barabara kwa kiwango cha lami kutoka Same-Kisiwani hadi Mkomazi hatua inayosaidia wananchi kufanya shughuli zao za uzalishaji katika mazingira rafiki.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI